KUHUSU KESI YA KANISA LA MCHUNGAJI RWAKATARE KUBOMOLEWA


Mchungaji Getrude Rwakatare.

Baraza la Usimamizi wa Mazingira (Nemc) limewasiliana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kesi ya kutaka kubomoa nyumba ya Mchungaji Getrude Rwakatare iliyomalizika kwa kutohusishwa baraza hilo ilirudi mahakamani ili haki itendeke.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana juu ya changamoto ya miji inayokuwa kwa kasi na usimamizi wa sheria za mazingira, Mkurugenzi wa Nemc, Bonaventure Baya, alisema kigogo mmoja wa Nemc ambaye amesimamishwa kazi alifanya uamuzi bila kuhusisha baraza na kushiriki maamuzi ambayo siyo sahihi katika kesi hiyo iliyoendeshwa kwa muda wa mwaka mmoja.

Alisema Nemc ilipotaka kuchukua hatua dhidi ya nyumba ya Rwakatare ilipelekwa mahakamani na kesi hiyo iliendeshwa kwa mwaka mmoja, lakini kigogo huyo akafanya maamuzi mwenyewe na kuficha nyaraka muhimu za kesi, hali iliyosababisha kufutwa.

“Baada ya kuwasiliana na Mwanasheria Mkuu tumeambiwa baada ya siku 10 utaratibu utakuwa umekamilika na kesi itaanza tena," alisema.

Katika hatua nyingine, Nemc imewatoza faini na kutoa onyo kwa makanisa, kampuni, taasisi na hoteli ambazo zimekaidi agizo la kuacha kupiga kelele licha ya wengi kugoma kulipa na kukimbilia mahakamani kwani sheria inawataka kufanya hivyo.

Aidha, Mkurugenzi huyo wa Nemc aliitaka serikali kuboresha huduma ya mipango miji ili kudhibiti ujenzi holela, mipango izingatie uwezo wa kada tofauti za wananchi, 'master plan' zizingatiwe na ihamasishe sekta binafsi kuwekeza katika ujenzi wa miundombinu ya kudhibiti taka za aina zote.

CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post