HII NDIYO KAULI YA MBOWE KUHUSU LOWASA NA CHADEMA




Mwenyekiti wa Chadema-Taifa Freeman Mbowe amesema, Edward Lowassa, aliyekuwa mgombea wa chama hicho kwenye Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana na kuungwa mkono na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), hakutoa hata senti moja alipojiunga na chama hicho.


Mbowe amezungumza hayo kwenye Mkutano wa Baraza Kuu la Chadema linaloendelea hivi sasa Jijini Mwanza.


Amesema kuwa, pamoja na kuwepo kwa kauli nyingi kwamba, Lowassa alimwaga pesa kabla ya kujiunga na chama hicho, ukweli unabaki kuwa hakutoa pesa yoyote kama ilivyokuwa ikidaiwa.


“Watoto wangu walikuwa wanakula sana maharage, sasa siku moja wakala nyama, jirani akasema umeona Lowassa kaja Chadema,” amesema Mbowe.


Akizungumzia migogoro ya kichama iliyokuwa imejitokeza kwenye uchaguzi uliopita Oktoba 25 mwaka huu Mbowe amesema, kuna kila sababu kushughulikia migogoro hiyo kwa haraka.


“Migogoro mingi ndani ya Chadema imepelekea kuanguka kwa chama, hivyo itashugulikiwa kwa haraka,” amesema na kuongeza; “Uchaguzi mkuu wa chama ni Oktoba 2018.”


Amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba, harakati za kisiasa hasa kukikuza chama ni gharama kubwa, jambo ambalo chama kinajitahidi kukabiliana nalo.


Amesema kwamba, pamoja na mambo yote ndani ya chama hicho lakini suala la rushwa haliwezi kuvumiliwa hata mara moja.


Akifafanua kauli hiyo amesema, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimeishi kwa kulea rushwa na kwamba, hali hiyo ndio imekifikisha hapo kilipo sasa.


Amesema, hali hiyo inaelekea kuingia Chadema jambo ambalo linaweza kusababisha kupasuka kwa chama hicho endapo halitashughulikiwa.


“Jambo ambalo hatutalivumilia ndani ya Chadema ni swala la rushwa kwani rushwa inagawa taifa, sasa swala la rushwa lililelewa na CCM na sasa inataka kuingia Chadema,” amesema.


“Kuna majimbo kama Iringa, Rukwa, Arusha Chadema waliachiwa kwa asilimia mia moja na Ukawa lakini kwanini wameshindwa kuchukua ushindi wa kutosha katika majimbo hayo?” amehoji.


Akizungumzia changamoto za Ukawa, Mbowe amekiri kuwepo na kwamba hakuna sababu ya kuzikwepa.

“Changamoto zilizopo ndani ya Ukawa hakuna haja ya kuzikimbia bali ni kupambana nazo,” amesema.


Akizungumzia umoja wa kitaifa amesema kwamba Chadema hakikubaliani na mtu yoyote anayetaka ama kushabikia kauli za kuligawa taifa.


“Nawashauri tunapokuwa popote lazima tukatae nchi yetu kugawanyika vipande vipande. Hatukotayari kufanya kosa kama hilo wala kushabikia kuligawa taifa ,” amesema.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527