ANGALIA PICHA-MAGUFULI AKIWAONGOZA VIONGOZI WA AFRIKA MASHARIKI KUWEKA JIWE LA MSINGI BARABARA YA ARUSHA HADI KENYA



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Kenya Mheshimiwa Uhuru Muigai Kenyatta, wameweka jiwe la msingi katika ujenzi wa barabara ya Arusha - Holili - Taveta - Voi, yenye urefu wa kilometa 234.3 ambayo inaunganisha nchi za Tanzania na Kenya.


Hafla ya uwekaji wa jiwe hilo la Msingi imefanyika jana katika eneo la Tengeru Mkoani Arusha na kuhudhuriwa na viongozi wengine wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambao ni Rais wa Jamhuri ya Uganda Mheshimiwa Yoweri Kaguta Museveni, Makamu wa pili wa Rais wa Jamhuri ya Burundi Dkt. Joseph Butore, Mwakilishi wa Rais Paul Kagame wa Jamhuri ya Rwanda ambaye ni Waziri wa Afrika Mashariki wa Rwanda Mheshimiwa Valentine Rwabiza na Makamu wa Pili wa Rais Sudan Kusini Mheshimiwa James Wan Iga.


Uzinduzi huo pia umehudhuriwa na Rais wa Zanzibar Dkt. Ali Mohamed Shein.


Kwa upande wa Tanzania ujenzi wa barabara hiyo unatakelezwa kwa awamu mbili ambapo awamu ya kwanza inahusisha ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Arusha hadi Tengeru yenye urefu wa kilometa 14.1, na ujenzi wa barabara ya mzunguko yaani "Bypass" yenye urefu wa kilometa 42.4.


Awamu ya pili itahusisha ujenzi wa barabara ya njia nne kuanzia Tengeru hadi Usa River yenye urefu wa kilometa 8.2 na Kutoka Usa River hadi Holili mpakani mwa Kenya na Tanzania yenye urefu wa kilometa 100.2


Gharama za upanuzi wa barabara ya Arusha - Tengeru na barabara ya kuzunguka nje ya jiji la Arusha kwa upande wa Tanzania ni shilingi bilioni 209.6, ambapo kati ya fedha hizo Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) itatoa mkopo wa shilingi bilioni 190.2 na serikali ya Tanzania itatoa shilingi Bilioni 19.4.


Aidha Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki ipo kwenye mazungumzo na serikali ya Japan ili kupata mkopo wa ujenzi wa awamu ya pili inayoanzia Tengeru hadi Holili.


Kwa upande wa Kenya, mradi huu unahusisha ujenzi wa barabara mpya kwa sehemu ya Taveta hadi Mwatate yenye urefu wa kilometa 100. Sehemu ya Mwatate hadi Voi ujenzi wake umekamilika.


Akizungumza katika hafla hii, Rais Dkt. John Pombe Magufuli ambaye ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, amesema wananchi wa Afrika Mashari hawapaswi kuwa masikini na kueleza kuwa mradi huo na mingine itakayotekelezwa chini ya ushirikiano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki itasaidia kuinua hali ya maisha ya wananchi.


Kwa upande wao Marais Uhuru Muigai Kenyatta wa Kenya, Yoweri Kaguta Museveni wa Uganda na wawakilishi wa marais wa Burundi, Rwanda, Sudani Kusini wameuelezea mradi huo kuwa ni moja ya miradi muhimu ya kuimarisha uchumi wa jumuiya ya Afrika Mashariki na wametoa wito kwa nchi zote wanachama wa jumuiya hiyo kushirikiana kukuza biashara baina yake.


Viongozi hao wote wamekiri kuwa Jumuiya hii yenye watu zaidi ya milioni 160, inayo nafasi ya kupiga hatua kubwa za kiuchumi na kuondokana na umasikini, ikiwa italitumia vizuri soko la pamoja kwa kubadilisha bidhaa kutoka nchi moja hadi nyingine na kujenga viwanda vingi badala ya kuendelea kutegemea bidhaa kutoka nje.


Gerson Msigwa
Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, IKULU
Arusha
03 Machi, 2016









Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527