MAGUFULI AJA NA MPYA: MAFISADI WAKINISHINDA MSINIITE RAIS,WALIOTUMBULIWA SI WENGI HATA HAWAJAFIKA 2000Rais Dk. John Magufuli amesema amejitolea kuwa sadaka kwa Tanzania katika vita dhidi ya mafisadi na kwamba akishindwa kufanya hivyo, hakuna sababu ya yeye kuitwa rais.

Pia amesema wote waliotumbuliwa majipu watafikishwa mahakamani ili sheria ichukue mkondo wake.

Akizungumza jana katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi katika sehemu ya barabara ya Sakina hadi Tengeru yenye urefu wa kilomita 14.1, itakayokuwa na njia nne, alisema ataendelea kutumbua majipu kwa kuwa wanaonufaika na kudidimiza uchumi wa nchi ni wachache.

“Tumeanza kuchukua hatua ndogo ndogo, tunatumbua majipu. Mpaka sasa waliotumbuliwa si wengi kiasi hicho, hawajafika hata 2,000. Juzi juzi nimesikia baadhi ya watu wameanza kuwatetea wanaotumbuliwa, nasema hao wanaowatetea washindwe na walegee,” alisema.

Hafla hiyo ilihudhuriwa pia na Rais Yoweri Museveni wa Uganda, Uhuru Kenyatta wa Kenya, Makamu wa Pili wa Rais wa Burundi, Dk. Joseph Butore, Makamu wa Pili wa Rais wa Sudan Kusini, James Wani Igga, Balozi wa Japan nchini na mwakilishi wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB).

Alisema wananchi wa Tanzania kwa muda mrefu wamekuwa wakipata shida na taabu kutokana na wachache kufilisi mali na rasilimali za nchi.

“Ifike mahali mmoja lazima ajitolee kufanya kazi hii. Mimi nimeamua kuwa sadaka kwa Tanzania, lazima tufanye kazi ya kutumbua majipu na kuwaletea maendeleo wananchi.

“Nisipofanya hivyo, hakuna sababu ya mimi kuitwa Rais. Hii nasema kwa dhati kabisa kutoka moyoni mwangu, naomba Watanzania waniombee,”alisema.

Alisema kwa mfano yapo mambo ya hovyo ambayo hivi karibuni Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), imeisababishia serikali upotevu wa fedha za matumizi ya simu nje ya nchi husika (roaming) kiasi cha Sh. bilioni 200.

Alisema watu wote wanaojihusisha na ufisadi watafukuzwa na kufikishwa mahakamani mwishowe kufungwa ili nao wakapate machungu.

“Hii nchi ilifika mahali ikawa kama shamba la bibi vile,” alisema na kusisitiza kuwa katika kuwaletea wananchi maendeleo hatafanya ubaguzi wowote kwa kuzingatia vyama, dini, kabila ila atachapa kazi tu.

“Nawaomba Arusha tujenge umoja wetu, tusibaguane. Tukianza kujenga umoja wa Tanzania na tukaunganishaa na umoja wa Uganda, Kenya, Burundi, Rwanda na Sudan Kusini, Jumuiya ya Afrika Mashariki itakuwa na maendeleo ya kasi," alisema Rais Magufuli ambaye ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Aliongeza kuwa: "Tukiamua tunaweza kubadilika na kuwaletea wananchi wa jumuiya hii maendeleo makubwa.”
Alisema wananchi wa EAC wanachohitaji si vyama ila kazi, maendeleo na maisha mazuri na si kuwafanya wachache wawe wanafaidi kuliko wengine.

Awali, alimpongeza Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema), kwamba ni mtu mchapakazi.

“Nampongeza sana Nassari, ni kijana safi anachotaka ni kazi na ameweza kuwaletea maendeleo wananchi wa jimbo lake.

Sipendi kuwa mnafiki, nampongeza sana Nassari. Ukimtazama usoni Nassari ni Chadema lakini kwa kweli moyo wake uko CCM,” alisema na kufanya umati wa watu kulipuka kwa shangwe.

Mapema Rais Museveni alisema: “Tukiwa tunazungumzia uchumi wa kisasa, Afrika hakuna umaskini, ina utajiri mwingi wa raslimali isipokuwa inakosa maendeleo tu.

“Ardhi ipo, madini yapo, lakini tunashindwa kuzitumia, hivyo tunakosa maendeleo, tunakosa elimu na tuna afya duni,” alisema.

Aliwataka wananchi kujikita katika kilimo cha kisasa badala ya kulimia tumbo peke yake.

Museveni alisema sekta ya kilimo, viwanda, huduma na ICT, ndizo zinazoweza kuleta maendeleo kwa nchi za EAC.

Hata hivyo, alisema shida ya Waafrika ni kulala na kwamba wanalala huku kukiwa kumekucha na kusisitiza kuwa:
“Tukiamka sisi sote tutakuwa na maendeleo kutokana na uzalishaji mkubwa utakaokuwapo," alisema.

Aliwaondoa wananchi hofu ya kupatikana kwa soko pale aliposema jumuiya hiyo ina watu zaidi ya milioni 160, hivyo idadi hiyo ni soko kubwa kwa bidhaa zitakazokuwa zikizalishwa na wananchi.

Kwa upande wake, Rais Kenyatta, alisema, viongozi wa jumuiya hiyo ndio waliofanya kazi ya kulala wakati kumekucha.
Alisema kazi kubwa waliyonayo wao ni kuwaletea maendeleo wananchi kwa kujenga miundombinu.

Aliwataka viongozi wenzake kubadilika badala ya kuwa na maneno mengi na kwamba sasa wawe watu wa kazi ambayo itawawezesha wananchi kupata maendeleo na kuyafurahia.

CHANZO: THE GUARDIAN

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post