NAIBU KATIBU MKUU CUF AHMED MAZRUI AHOJIWA NA POLISI ZANZIBAR,ASKARI WENYE SILAHA WAFANYA DORIA MITAANI




Wakati polisi visiwani Zanzibar wakimhoji Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Nassor Ahmed Mazrui jana, ulinzi uliimarishwa mjini Unguja huku askari wenye silaha na magari ya deraya wakifanya doria mitaani.

Mazrui, ambaye alifika makao makuu ya jeshi hilo saa 2:00 asubuhi akiambatana na wakili wake, ndiye aliyekuwa mkuu wa timu ya kampeni ya mgombea urais wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, katika uchaguzi uliofanyika tarehe 25 Oktoba 2015, ambao chama chake kinaamini kuwa kilishinda.


Barabara zinazoelekea makao makuu ya polisi kutokea Jang’ombe, Kilimani na Bomani zilifungwa huku vikosi vya ulinzi na usalama vikiwa vimetapakaa maeneo hayo na mitaa mbalimbali mjini Unguja.


Wakazi wa Zanzibar wanaojiandaa kwa uchaguzi wa marudio uliopangwa kufanyika Machi 20, kuanzia Jumatano mchana walishuhudia askari wenye sare wakiwa katika magari maalumu ya kijeshi wakirandaranda kwenye barabara za Unguja, hususan mitaa ya Ng’ambo kupitia Mnazi Mmoja, Darajani, Amani, Chumbuni na Mtoni kuelekea Bububu.


Wakati hali ikionekana hivyo mitaani, Mazrui alikuwa ndani ya Ofisi ya Upelelezi ya Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Ziwani mjini Unguja ambamo alihojiwa kwa saa tatu na nusu.


Alianza kuhojiwa tangu saa 2.00 asubuhi kama alivyotakiwa na jeshi hilo kuripoti kupitia barua ya wito aliyotumiwa hivi karibuni, hadi saa 5.30


Hata baada ya kumaliza kuhojiwa, Mazrui aliyekuwa waziri wa biashara, alilazimika kubaki kituoni hapo akisubiri kukamilika kwa taratibu za dhamana. Aliruhusiwa kuondoka saa 6.40 mchana.


Pamoja na ulinzi kuimarishwa, mamia ya wananchi, hasa wapenzi, wanachama na wafuasi wa CUF, walifika makao makuu ya chama hicho yaliyoko Mtendeni ili kumpokea Mazrui akitokea polisi.

Baada ya kuachiwa kwa dhamana, Mazrui alisema alihojiwa na polisi kuhusu kauli aliyoitoa hivi karibuni alipokuwa Dunga Kiembeni, Wilaya ya Kati mkoani Kusini Unguja kwamba chama chake cha CUF kimechoshwa na vitendo vya hujuma na vya kihuni dhidi ya mali na ofisi zao.


“Naam, nimewaambia kwamba hiyo ni kauli yangu na niliyesema hayo ni mimi kuwa CUF tumechoshwa na uhuni huo,” alisisitiza Mazrui mara baada ya kuachiwa kwa dhamana ya masharti ya kuwa na wadhamini wawili na kila mmoja wao kutakiwa kuweka hapo Sh500,000.


“Wamesema nimetoa kauli za uchochezi hivyo watanishtaki mahakamani na wamenitaka niripoti polisi Jumanne na Alhamisi.” Alisema

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527