Waziri wa Afya awasimamisha wakurugenzi wanne MSD



Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Watoto na Wazee Mhe. Ummy Mwalimu amewasimamisha wakurugenzi wanne toka Bohari ya Dawa ya Taifa(MSD) kwa ubadhilifu wa fedha takribani Shillingi Billion 1.5.

Ameyasema hayo wakati akizungumza na Waandishi wa Habari katika Kitengo cha Afya ya Mama na Mtoto baada ya kupokea vifaa toka Bohari Kuu ya Dawa ya Taifa (MSD), amesema amepata taarifa ya uchunguzi ofisini kwake ya ubadhilifu wa kiasi hicho cha fedha na kuamua kuwasimamisha wakurugenzi wanne kupisha uchunguzi.

“ Nimeletewa taarifa ofisini kwangu na nimeamua kuchukua fursa hii kuwaambia na hili pia kwamba nimewasimamisha wakurugenzi wanne toka Bohari ya Kuu Dawa ya Taifa kwa ubadhilifu wa fedha na nisingeweza kusubiri nitumbuliwe mimi jipu na Mhe.Rais kwahiyo nimeamua kuwachukulia hatua kwa kuwasimamisha kazi ili kupisha uchunguzi kuendelea”

“ Hizi ni zama za kufanya kazi na kuwajibika sasa inabidi tuwajibike kwa kufanya kazi na hatutowavumilia watendaji watakaoenda kinyume na utaratibu katika ofisi yoyote ile katika sekta ya afya na tutawachukulia hatua kwani tunataka uwajibikaji ili kuiendeleza sekta ya Afya ambayo ni muhimu sana kwa kila mwanadamu” Alisema Ummy.

Amewataja aliowasimamisha kazi kuwa ni Joseph Tesha Mkurugenzi wa Fedha na Mipango, Misanga Muja Mkurugenzi wa Ugavi, Heri Mchunga Mkurugenzi wa Manunuzi na Cosmas Mwaifani Mkurugenzi Kanda na Huduma kwa Wateja ambapo amewataka Mkurugenzi na Mwenyekiti wa Bodi ya Bohari ya Dawa ya Taifa kuwaandikia barua mara moja ya kuwasimamisha kazi.

Katika kuboresha sekta ya Afya nchini, Wizara wa Afya ,Maendeleo ya Jamii,Jinsia,Watoto na Wazee imejipanga kufanya kazi kwa taratibu na misingi iliyopo ili kuhakikisha inapeleka mbele gurudumu la maendeleo hasa katika sekta ya afya.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527