UKAWA WATOA TAMKO BAADA YA UCHAGUZI WA MEYA WA JIJI LA DAR KUAHIRISHWA TENA






Uchaguzi Mkuu ulifanyika tarehe 25.10.2015 na wananchi wa Jiji la DSM Waliamua kuongozwa na UKAWA na ndio maana walichagua Madiwani na Wabunge wengi kutoka UKAWA. Kati ya Majimbo 10 ya Uchaguzi katika Jiji la DSM CCM ilipata Majimbo 3 tu baada ya kuchakachua na UKAWA ilipata yaliyosalia.


Hali ni hiyo hiyo kwenye kata. Wananchi waliamua kuipumzisha CCM kwa kuwa walikua wamechoshwa na uendeshaji mbaya wa Jiji la Dar es Salaam . Tangu Uchaguzi umalizike mpaka leo wananchi wanakosa huduma za Jiji kwa sababu CCM ilitaka kushinda Umeya wa Jiji kwa staili ileile waliyozoea ya goli la mkono.

Mara wakaletwa wapiga kura feki kutoka Zanzibar huku Wakijua wazi kuwa TAMISEMI sio jambo la Muungano. Waziri mwenye dhamana na TAMISEMI hajawahi kutoa kauli wala kukemea hali hiyo hata siku moja huku akijua wazi kuwa vitendo hivyo vilikua ni kinyume Cha sheria za Nchi.



Leo tarehe 27.02.2016 tumeshuhudia Uchaguzi ukiitishwa na baada ya wajumbe Kuwasili wakakutana na kilichoitwa zuio la Mahakama la Tangu tarehe 05.02.2016 .



Jambo hili limetokea baada ya Taarifa kusambaa jana tarehe 26.02.2016 kuwa CCM walipeleka shauri mahakamani la kuweka zuio na kuwa shauri hilo lilitupiliwa Mbali.



Nini kinafichwa Jiji la DSM ? 
Tuna taarifa kuwa ni Ufisadi mkubwa uliofanywa na viongozi wa Jiji waliopita na wakishirikiana na Viongozi wa CCM kupora Mali za Jiji kama vile UDA, Mali za soko la Kariakoo, Viwanja na majengo ya Jiji.


Pili tuna Taarifa kuwa hawataki majipu ya Jiji yatumbuliwe kwani kuna vigogo wakubwa wa CCM watatumbuliwa kutokana na kushiriki kwenye Ufisadi mkubwa ndani ya Jiji la Dar es Salaam . Mipango iliyopo.


Mkutano wa Uchaguzi Leo uliitishwa pamoja na kuwepo hicho kinachoitwa zuio la Mahakama kwa lengo la kuwaudhi Madiwani wa UKAWA ili waonekane kuwa wanafanya fujo .


Hii ni kutokana na ukweli kuwa kama zuio lipo Tangu siku CCM wanaadhimisha miaka39 ya kuzaliwa kwake ni kwanini Mkurugenzi aliitisha mkutano wakati akijua Mahakama imeweka zuio?.


Mpango huu umesukwa ili kuhakikisha kuwa Waziri mwenye dhamana na TAMISEMI anatengenezewa sababu za kuweza kuvunja Halimashauri ya Jiji la Dar es Salaam na kuunda Tume ya kuongoza Jiji.



Ni vyema tukaweka angalizo mapema kuwa Mafisadi wana mikakati mingi sana ya kuhakikisha kuwa hawatumbuliwi Majipu. Kama Rais ambaye ndio Waziri mwenye dhamana na TAMISEMI hakubaliani na mbinu hizi za Mafisadi, aingilie Kati Mara moja na kuhakikisha kuwa Uchaguzi wa Meya unafanyika na kazi ya kutumbua majipu ya Jiji inaendelea kama ambavyo imeshaanza katika Manispaa za Ilala na Kinondoni zinazoongozwa na UKAWA .
Imetolewa na John Mrema.

Mkurugenzi wa Bunge na Halimashauri CHADEMA.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527