Kimenuka!! SASA ASKARI WA JWTZ KUINGIA MSITUNI KUWASAKA MAJAMBAZI WANAOTISHIA AMANI

Siku moja baada ya majambazi 12 yenye silaha kuvamia tawi la benki ya Access la Mbagala Rangi Tatu jijini Dar es Salaam na kuua kisha kupora Sh. milioni 20, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Charles Kitwanga, ametangaza uwezekano wa kutumia Jeshi la Wananchi (JWTZ) kusaka wahalifu wote.
 
Katika tukio hilo watu sita waliuawa, ambao ni majambazi watatu, polisi mmoja na raia wawili.

Waziri Kitwanga alitangaza mkakati huo jana katika Kituo cha Polisi Kati, wakati wa mkutano na waandishi wa habari wa kuzungumza tukio hilo ambalo majambazi tisa walitokomea msituni na fedha walizopora.

“Tumeamua kujipanga upya, ikiwezekana tutumie askari wa JWTZ ili tufagie misitu yote ya Bagamoyo, Pwani kama kuna makambi yao huko tuyaondoe yote,” alisema na kuongeza:

“Majambazi hayo na mengine yasidhani kwamba Jeshi la Polisi limelala, tutawamaliza wote na tutatumia nguvu zetu zote kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na katika operesheni hii tunawaomba wananchi wawe watulivu. Wasione kama tunawabughudhi.”

WATUMIA PIKIPIKI
Kitwanga alisema katika operesheni hiyo watakuwa wakiwasimamisha mara kwa mara watumia pikipiki kwa ajili ya ukaguzi ili kuwatambua wenye nia njema na waovu.

“Tunafanya hivi kwa sababu katika tukio hili la Benki ya Access wahalifu hawa 12 walitumia pikipiki 6 na vyombo hivi vya usafiri vimekuwa vikitumiwa na majambazi sana katika kufanikisha matukio yao,” alisema Waziri Kitwanga.
Aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano na kama wana tetesi zozote za wahalifu maeneo yao walijulishe jeshi hilo ili wakamatwe mara moja.

SINEMA YA UPORAJI MBAGALA
Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Kamishna wa Polisi, Simon Sirro alisema juzi mchana majambazi hao wakiwa na bunduki ya SMG na mabomu matatu ya kutupa kwa mkono yaliyotengenezewa Russia, walifika kwenye benki hiyo wakiwa na pikipiki sita.

Alisema kila pikipiki ilikuwa na majambazi wawili na baada ya kuwasili eneo hilo waliwashambulia polisi waliokuwa nje wakilinda benki hiyo.

“Walivamia chumba cha askari nje ya benki na kumuua kwa kumpiga risasi kichwani askari wetu na kumjeruhi mwingine maungoni, kisha walichukua silaha yake na kuingia nayo ndani ya benki,” alisema.

Alisema baada ya kuingia ndani, walimshambulia mlinzi wa kampuni binafsi ya Security Group Afrika, Baraka Fredrick, maarufu kama Selemia, ambaye alifariki papo hapo.

Pia alisema majambazi hao waliwashambulia kwa kuwajeruhi kwa risasi wafanyakazi wawili wa benki hiyo ambao ni Ofisa Mikopo, Salum Juma na Francis Amani waliokuwa Chumba cha Kuhifadhia Fedha (Strong Room).

“Walipiga ‘safe’ ya kuhifadhia fedha lakini haikufunguka ndipo wakaamua kwenda kaunta na kufanikiwa kupata (Sh.) milioni 20 na kuondoka nazo.”

Alisema wakati wanaondoka walifyatua risasi iliyompata kidevuni Abdi Salum maarufu kama Shemdoe, ambaye ni muuza duka jirani na benki hiyo.

Sirro alisema kwa sababu Jeshi lake limejiimarisha kiulinzi maeneo hayo, vikiwemo vikosi vya farasi, pikipiki na magari, walianza kuwafuatilia majambazi hao ambao wakati huo walikuwa wakitumia usafiri wa pikipiki.

Alisema katika majibizano ya risasi, waliwaua majambazi watatu na kufanikiwa kupata SMG tatu na pikipiki sita.
Alisema majambazi wengine walikimbia kwa miguu na kuziacha pikipiki hizo lakini fedha ambazo zimeibwa hawakufanikiwa kuzipata.

Sirro alisema vikosi vyake viliendelea kuwafukuza majambazi wengine hadi msitu wa Kongowe unaotokea mkoa wa Pwani lakini yalitokomea ndani ya msitu huo na polisi wanaendelea kuyasaka.

Polisi walishindwa kuwapiga risasi majambazi hao wakati wakiwakimbiza kwa kuhofia kujeruhi wananchi, alisema.

“Ili kuonyesha majambazi hawa walikuwa wamejipanga, walivamia wakiwa na mabomu ili waliovamiwa wasipate msaada, askari wetu aliyejeruhiwa ambaye amelazwa Muhimbili alifanya kazi kubwa licha ya majeraha aliyopata.”

CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post