DEREVA AFARIKI AKIOGELEA MTONI HUKO RUVUMA

Dereva wa Kampuni ya SYNOHYDRO inayojenga kwa kiwango cha lami barabara ya kutoka Tunduru Mjini kwenda katika tarafa ya Nakapanya Wilayani humo mkoani Ruvuma, amefariki dunia baada ya kusombwa na maji ya Mto Muhuwesi.

Dereva huyo, Ally Ramadhani (31), alikumbwa na mkasa huo Alhamisi saa 11.30 jioni wakati akioga katika mto huo.
Taarifa zilizopatikana zilisema kuwa marehemu alikwenda kuoga katika mto Muhuwesi baada ya muda wa kazi kwisha na kwamba aliteleza na kutumbukia mtoni na kusombwa na mkondo mkali wa maji.

Taarifa hizo zilisema kuwa baada ya kuanguka, marehemu alisikika akiomba msaada wa kuokolewa lakini kwakuwa wenzake walikuwa hawajui kuogelea waliogopa kujitosa majini.

Mtu aliyekuwa na marehemu na ambaye aliomba jina lake lisitajwe , alisema dereva huyo alizama katika maji hayo na hakuonekana tena.

Diwani wa kata ya Muhuwesi, Nurdini Mnolela, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo na kwamba baada ya taarifa hizo kuwafikia, alianzisha msako wa kuutafuta mwili wa marehemu kwa pamoja na watu waliojitolea wakiwa wanafuata mto huo.

Mnolela aliendelea kufafanua kuwa, hata hivyo, kazi hiyo imekuwa ngumu kutokana na wananchi wengi kutokuwa na ujuzi wa kupigambizi. Huenda zoezi la kutafuta mwili likachukua muda mrefu, alisema.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ruvuma, Zubery Mombeji, alithibitisha tukio hilo na kwamba ametuma kikosi kwenda kushirikiana na wananchi katika msako huo. 
Chanzo-Nipashe Jumapili

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527