RADI YAUA WAWILI,KUJERUHI WATATU HUKO KATAVI WALIKUWA CHINI YA MTI SHAMBANI MVUA IKINYESHA
Watu wawili Lupimwa Julias(30) na Remi Madirisha (32) wakazi wa Kijiji cha Ilebula Tarafa ya Kabungu Wilaya ya Mpanda mkoani Katavi wamekufa hapo hapo baada ya kupigwa na radi na wengine watatu kujeruhiwa wakati wakiwa shambani.Tukio la vifo vya watu hao wawili lilitokea juzi majira ya saa kumi na nusu jioni kijijini hapo wakati watu hao wakiwa shambani kwao.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Katavi Dhahiri Kidavashari amesema watu watatu waliojeruhiwa na radi hiyo kuwa ni Tatu Jerald ,Stela John na Filiberti Paskali wote wakazi wa Kijiji cha Ilebula Wilayani hapa.Alisema kabla ya tukio hilo marehemu hao wawili na majeruhi walikuwa shambani kwao wakiwa wanalima shamba lao lililiopo kwenye Kijiji hicho.


Wakati wakiwa wanaendelea kulima mvua ilianza kunyesha ambapo wote waliamua kwenda kujikinga chini ya mti uliokuwa kwenye shamba lao.

Kamanda Kidavashari alieleza ndipo watu hao radi ilipowapiga na kupelekea vifo vya watu wawili na kujeruhi watatu.


Alisema baada ya tukio majeruhi wote watatu walipelekwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mpanda na wanaendelea na matibabu katika wodi namba moja walikolazwa huku hali zao zikiwa zinaendelea vizuri .

Amesema miili ya marehemu wamekabidhiwa ndugu wa marehemu kwa ajili ya mazishi.


Kamanda Kidavashari amewatahadharisha wananchi wa Mkoa wa Katavi kuwa makini katika kipindi hiki cha masika pindi mvua zinaponyesha kujihifadhi maeneo yaliyo salama.
Na Walter Mguluchuma-Malunde1 blog Katavi

Download/Pakua App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527