JELA MIAKA MITANO KWA WIZI WA MBUZI..BADO ANA KESI YA WIZI WA KUKU 23








MAHAKAMA ya Mwanzo Vwawa mjini wilayani Mbozi mkoani Mbeya imemuhukumu Patrick Moses(19) mkazi wa Ilembo kutumikia jela miaka mitano baada ya kukiri kosa la kuiba Mbuzi mmoja mwenye thamani ya Sh 85,000 mali ya Bahati Mtafya.

Akisoma hukumu hiyo hakimu wa mahakama hiyo,Lazima Mwaijega alisema kutokana kifungu cha sheria 268 na mshitakiwa kukiri kosa hivyo mahakama imeamuru mshitakiwa kutumikia kifungo hicho ili iwe fundisho kwake na kwa wengine wenye nia ya kutenda kosa kama hilo.

Mshitakiwa alipopewa nafasi ya kujitetea aliiomba mahakama kumpunguzia adhabu kwani anategemewa na familia yake,hata hivyo hakimu Mwaijega amesema kifungo hicho cha miaka mitano amepunguziwa pia kwa kuwa ni kosa lake la kwanza.

Awali imeelezwa mahakamani na mwendesha mashitaka wa polisi Hamis Mohamed kuwa January 20,mwaka huu saa 11 jioni mshitakiwa alivamia nyumbani kwa Bahati Mtafya (38) na kuiba mbuzi mmoja mwenye thamani ya Sh. 85,000 huku akijua kufanya vyo ni kosa kisheria namba 229 sura ya 16 kanuni ya adhabu.

Aidha mwendesha mashitaka huyo aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa mshitakiwa ili iwe fundisho kwake na kwa wale wenye nia ya kutenda kosa kama hilo kutokana na wimbi kubwa la vijana kujikita katika wizi na kuacha kufanya kazi halali.

Katika hatua nyingine mshitakiwa huyo alipandishwa kizimbani hapo kujibu tuhuma ya wizi wa kuku 23 wenye thamani ya Sh laki 4 mali ya Evance Mwakenja mkazi wa Ilembo Vwawa .

Imeelezwa mahakamani hapo na mwendesha mashitaka wa polisi Hamis Mohamed kuwa tukio hilo lilitokea Januari 20 mwaka huu saa 8 usiku ambapo mshitakiwa aliiba kuku 23 wenye Thamani ya Sh.laki 4 mali ya Evance Mwakenja huku akijua kufanya hivyo ni kosa kisheria.

Hata hivyo mshitakiwa alikana shitaka linalomkabili na hakimu wa mahakama hiyo Chirstina Mlwilo amesema shauri hilo litaanza kusikilizwa Januari 27 mwaka huu,pia hakimu huyo amesema dhamana ya shilingi laki 4 kwa mshitakiwa ipo wazi pamoja na kuwa na wadhamini wawili wenye vitambulisho vya mpiga kura.

Hata hivyo mshitakiwa amerudiswa mahabusu kwa kushindwa kutimiza masharti la dhamana ya shilingi laki nne hivyo kuanza kutumikia kifungo cha miaka mitano ya wizi wa mbuzi.

Na Ezekiel Kamanga wa JAMIIMOJABLOG

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527