BERNARD MEMBE: SIWEZI KUSTAAFU SIASA KWA SABABU HAINA MWISHOAliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe amesema hana mpango wa kustaafu siasa kwa sababu haina mwisho.

Pia, amesema kwa sasa anafanya kazi ya uandishi wa vitabu kwa lengo la kuwashirikisha na kuwarithisha Watanzania mazuri aliyonayo baada ya utumishi wake wa kisiasa wa miaka 35.

Membe alisema hayo katika mahojiano maalumu na Mwananchi yaliyofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.

Alisema anaandaa vitabu vinne vyenye maudhui tofauti. “Hilo la kuandika vitabu nimeshalianza, nina vitabu zaidi ya 265 nimehifadhi na kuvisoma katika maktaba yangu kuhusu mambo mbalimbali ya dunia, nami ninatengeneza vinne, muda ukifika nitatoa taarifa,” alisema Membe.

Waziri huyo aliyehudumu katika Serikali ya Awamu ya Nne katika wizara hiyo kwa miaka tisa, alisema kati ya vitabu anavyoandika viwili vitatoka mwaka huu.

“Kimoja cha maisha yangu, ni vitabu vizuri sana, nimekuwa mwanasiasa kwa miaka 35, nimejihusisha zaidi na masuala ya utatuzi wa migogoro barani Afrika... kitabu kingine kitahusu migogoro na Serikali za Afrika,” alisema.

Alitaja vingine kuwa ni kuhusu uongozi na cha mwisho kitahusu siasa za Tanzania kinachowalenga zaidi vijana kikieleza namna nchi inavyoweza kulinda heshima yake duniani.

“Nchi hii tumeirithi kutoka kwa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere. Yeye alikuwa mwana ukombozi halisi. Mwaka 1963 alianzisha harakati za ukombozi, Tanzania ikawa makao makuu ya nchi zote zinazopigania uhuru. Vyama vya ukombozi vikaweka makao makuu yake hapa, vingine vikaanzia harakati zake hapa,” alisema Membe.

Alisema sifa ya kwanza ya Tanzania duniani ni ukombozi na ilikuwa mwenyekiti wa nchi tano zilizokuwa mstari wa mbele katika ukombozi Kusini mwa Afrika.

Akizungumzia kuhusu hatima yake kisiasa, Membe aliyewania kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM kabla jina la Dk John Magufuli ambaye sasa ndiye rais kuteuliwa, alisisitiza kuwa siasa haina mwisho.

“Tafsiri ya siasa ni mchakato wa namna ya kuyashughulikia matatizo ya watu, usipoyashughulikia vizuri, utaibadilisha siasa kutoka kwenye amani kwenda kwenye mtafaruku,” alisema.

Akimnukuu aliyekuwa Rais wa Marekani, Bill Clinton, Membe alisema mwanasiasa mzuri duniani ni yule aliyeondoka kwa heshima na anayeheshimu familia yake.

Membe aliwataka wanasiasa walioshindwa katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 kuacha kujipenyeza na kuendeleza ubabe wa kisiasa, akisema kufanya hivyo ni sawa na upuuzi, badala yake wasubiri muda wao watakapochaguliwa.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post