Kimenuka !! CHADEMA WALIANZISHA SHINYANGA,WAMEANZA NA HII,KINACHOFUATA NI MAANDAMANO WAKIWA NA NDOO ZA MAJI KICHWANI


Hapa ni ndani ya ofisi ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo Chadema mkoa wa Shinyanga ambapo madiwani wa chama hicho wakiongozwa na mwenyekiti wa madiwani wa CHADEMA manispaa ya Shinyanga Emmanuel Ntobi wamekutana na waandishi wa habari kueleza kupinga kitendo cha mamlaka ya maji na usafi wa mazingira mjini Shinyanga (SHUWASA) kupandisha bei za maji kinyume na utaratibu unaotakiwa kufuatwa ikiwa ni pamoja na wananchi kutoshirikishwa.Kulia ni Emmanuel Ntobi,diwani wa kata ya Ngokolo (mwenyekiti wa madiwani wa Chadema)kushoto kwake ni diwani wa kata ya Masekelo Samwel SambayiMwenyekiti wa madiwani wa CHADEMA manispaa ya Shinyanga Emmanuel Ntobi akizungumza kwenye mkutano wao na waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga leo asubuhi.

Ntobi amesema Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA)katika manispaa ya Shinyanga kimejipanga kufanya maandamano ya amani yasiyo na kikomo siku chache zijazo huku wananchi wakiwa wamebeba ndoo za maji kichwani kupinga ongezeko la bei ya maji katika mji huo kutoka mamlaka ya maji na usafi wa mazingira Shinyanga mjini SHUWASA.


Ntobi amesema pamoja na kwamba wananchi wamekuwa wakilalamika tangu mwaka 2010 kuhusu ongezeko la bei ya maji, cha kushangaza baada ya uchaguzi kumalizika hivi karibuni bei ya maji imepanda maradufu yaani kutoka shilingi 790 kwa unit moja na sasa imepanda kufikia shilingi 1,105 kwa unit moja kwa mtumiaji wa nyumbani.
Kwa upande wa taasisi  amesema bei ya unit moja ya maji  ilikuwa shilingi 1,000 na sasa ni 1,500,nyumba za biashara unit moja shilingi 1,000 hadi 1,560,viwandani shilingi 1,110 sasa ni 2000 kwa unit moja pamoja na malipo ya gharama za matengenezo nazo zimepanda kutoka shilingi 2,000 hadi 2,500 kwa watumiaji wa majumbani pekee,huku kwa wateja wa kwenye taasisi kutoka shilingi 3,500 hadi 4,500,biashara 3,500 hadi 4,500 na viwandani kutoka 3700 hadi 10,000.Ntobi amesema hata gharama za kuunganishiwa maji upya (Re-connection) zimepanda kutoka shilingi 8000 hadi 10,000 kwa watumiaji wa majumbani na kutoka 10,000 hadi 20,000 kwa watumiaji wa viwandani.

Ntobi ambaye ni diwani wa Chadema kata ya Ngokolo amesema madiwani 7 wa Chadema katika manispaa ya Shinyanga wanaunga mkono jitihada za rais John Pombe Magufuli katika kuboresha maisha ya wananchi na kuiomba serikali  kusikiliza kilio cha muda mrefu cha wakazi wa Shinyanga kupunguziwa gharama za bei ya maji kwani ndiyo chanzo cha maisha magumu kwa wananchi.

Kulia ni katibu wa madiwani wa CHADEMA mchungaji Jilala Obed ambaye ni diwani wa kata ya Lubaga akizungumza katika mkutano huo ambapo ameitaka SHUWASA kuondoa gharama za maji kwani wanaumiza wananchi na maagizo hayo yasipotekelezwa wataitisha maandamano ya amani na wamejiandaa kuonana na mkuu wa wilaya ya Shinyanga,mkuu wa mkoa ,waziri wa maji na rais

ILI KUEPUKA KUANDIKA HABARI YA UPANDE MMOJA;Baada ya kutoka kwenye mkutano huo ulioitishwa na madiwani wa Chadema,waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga zaidi ya 10 walielekea kwenye ofisi za SHUWASA kwa ajili ya kuonana na mkurugenzi wa SHUWASA,Sylivester Mahore ili azungumzie suala la kupanda kwa gharama za maji/bei ya maji kutokana na madiwani na wananchi kulalamika mara kwa mara juu ya kitendo cha bei ya maji kuongezwa kinyemela tena bila kushirikishwa.

Hata hivyo juhudi za waandishi wa habari wakiongozwa na mwenyekiti wa klabu ya waandishi wa habari mkoa wa Shinyanga Kadama Malunde ziligonga mwamba baada ya mkurugenzi wa SHUWASA Sylivester Mahore aliyekuwa ofisini tena muda wa kazi kudai kuwa hana muda wa kuzungumza na waandishi wa habari kutokana na kazi nyingi alizokuwa nazo.
Waandishi wa habari wakiwa nje ya ofisi ya mkurugenzi wa SHUWASA wakimsubiria mwenyekiti wao Kadama Malunde atoke ndani ya ofisi ya mkurugenzi wa SHUWASA baada ya kuomba aonane na mwandishi wa habari mmoja tu!! Mkurugenzi huyo aliyeonesha kukerwa na ujio wa waandishi wa habari bila kupewa taarifa kabla(Appointment) alisema hawezi kuzungumzia suala la ongezeko la bei ya maji kwani alikuwa ana kazi zingine za kiofisi za msingi zaidi na badala yake akawataka waandishi wa habari waache kuvamia ofisi bila taarifa huku akitaka wakutane naye siku inayofuataWaandishi wa habari wakiwa nje ya ofisi ya mkurugenzi wa SHUWASAWaandishi wa habari wakiwa nje ya ofisi ya mkurugenzi wa SHUWASA huku wengi wakiwa eneo la mapokezi wakimsubiri mwenyekiti wao atoke ndani ya ofisi ya mkurugenzi wa SHUWASA kwani kulitokea hali ya kutoelewana takribani dakika 6 ndani ofisi hiyo

 

Ongezeko la bei ya maji kinyemela katika manispaa ya Shinyanga kimekuwa kilio cha muda mrefu huku wananchi wakidai kuwa uwepo wa mamlaka mbili zinazofanya kazi ya kusambaza maji katika mji huo yaani KASHWASA na SHUWASA zimekuwa zikivutana matokeo yake wananchi kuendelea kutumia gharama kubwa kupata huduma ya maji safi na salama.Ikumbukwe kuwa Kero ya maji ilikuwa ajenda ya kila mgombea katika uchaguzi mkuu uliopita na kila mmoja alipopanda jukwaani alijinadi kuwa akichaguliwa atahakikisha kuwa kero hiyo inakwisha...
Hapa kazi tu ndiyo kauli mbiu ya sasa Tanzania....Je ahadi hiyo itatekelezwa???
Na Mwandishi maalum wa Malunde1 blog Shinyanga

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527