ASKARI WA JWTZ WANYOFOLEWA MAENEO NYETI HUKO ZANZIBAR





Askari wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWTZ) waliokuwa wakilinda maeneo nyeti ya kiuchumi na kijamii Zanzibar tangu kufutwa matokeo ya uchaguzi mkuu Oktoba 28, mwaka huu, wameondolewa kuanzia juzi katika maeneo hayo.

Akari hao walikuwa wameimarisha ulinzi katika Bandari ya Malindi, Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, Kituo cha Matangazo cha Televisheni na Radio vya Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC), Mnara wa Kumbukumbu ya Miaka 50 ya Mapinduzi ya Zanzibar na Kiwanja cha Watoto cha Michezo cha Kariakoo.

Akizungumza na Nipashe mjini Zanzibar jana, Kamishina wa Jeshi la Polisi Zanzibar, Hamdan Omar Makame, alithibitisha askari wa JWTZ kuondokakatika maeneo hayo na jukumu la ulinzi kuchukuliwa na polisi.

Alisema mahitaji ta askari yanapokuwa makubwa hasa katika kipindi cha uchaguzi, katika baadhi ya malindo hulazimika kuchukuliwa askari wa JWTZ kwa madhumuni ya kuimarisha usalama zaidi katika maeneo hayo.

Alisema kutokana na hali ya Zanzibar kuwa shwari, askari wa JWTZ wataendelea na majukumu yao mengine na askari polisi kurudi katika malindo yao ya kawaida baada ya majukumu yao ya kazi kupungua tangu kufanyika uchaguzi mkuu Oktoba 25, mwaka huu.

Kamishna Hamdan alisema wakati wa shughuli za kitaifa au uchaguzi mkuu askari polisi wanakabiliwa na majukumu mengi ndiyo maana sehemu ya majukumu ya kazi zao huchukuliwa na askari wa JWTZ kwa muda yakiwemo malindo.

Hata hivyo, alisema pamoja na askari hao wa JWTZ kuondolewa katika maeneo hayo, lakini Makao Makuu ya Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (Zec) yataendelea kulindwa na askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania.

CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527