RAIS WA TANZANIA JOHN MAGUFULI AKUTANA NA RAIS WA ZANZIBAR DR SHEIN

 
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli leo amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein Ikulu Jijini Dar es salaam.

Akizungumza na vyombo vya habari mara baada ya mazungumzo hayo, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Ali Mohamed Shein amesema lengo la mazungumzo hayo ilikuwa ni kumpa taarifa Rais Magufuli juu ya hali ya mazungumzo ya kisiasa yanayoendelea huko Tanzania Zanzibar baada ya uchaguzi Mkuu.


Rais Shein amesema mazungumzo juu ya hali ya Zanzibar yanaendelea chini ya kamati maalum ambayo yeye ndiye mwenyekiti na wengine wakiwa ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, Makamu wa pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd, Rais Mstaafu wa awamu ya pili wa Jamhuri ya Muungo wa Tanzania Alhaji Ali Hassan Mwinyi, Rais Mstaafu wa awamu ya nne wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Rais Mstaafu wa awamu ya sita wa Zanzibar Dkt. Amani Abeid Karume na Rais Mstaafu wa awamu ya tano wa Zanzibar Dkt. Salmin Amour.


Amesema tayari kamati hiyo imeanza mazungumzo tangu tarehe 09 Novemba, 2015 na kwamba mazungumzo hayo yamelenga kujadili hatma ya Zanzibar baada ya uchaguzi Mkuu.


Rais Shein amebainisha kuwa mazungumzo hayo bado yanaendelea.


"Kwa hiyo nimekuja kumpa taarifa Mheshimiwa Rais Magufuli kuhusu maendeleo ya mazungumzo yetu ili aweze kujua kinachoendelea akiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo Zanzibar ni sehemu yake, na sisi ni jukumu letu kumpa taarifa hiyo" Alisema Rais Shein.


Aidha Rais Shein ameongeza kuwa mazungumzo hayo yatakapokamilika wananchi watajulishwa.


Chanzo-Mpekuzi blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527