Gari la maji ya kuwasha likiwa mtaani-Picha kutoka Maktaba ya Malunde1 blog
Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wilaya ya Shinyanga mjini kimesema kimefanikiwa kufanya maandamano yao ya amani kupinga matokeo ya uchaguzi mkuu 2015 yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi kupitia askari wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga.
Akizungumza na Malunde1 blog mapema leo katibu wa Chadema wilaya ya Shinyanga mjini George Kitalama amesema wamefanikiwa kufanya maandamano yao kupitia jeshi la polisi akidai kuwa polisi wameandamana badala ya Chadema wakiwa na magari yao mtaani.
Kitalama amesema walipanga kufanya maandamano mji mzima wa Shinyanga
lakini polisi ndiyo wamejitokeza kufanya maandamano kwa magari yao kila
mtaa katika wilaya ya Shinyanga.
“Chadema leo tumefanya maandamano ya aina yake,polisi
wametusaidia kuandamana na magari yao mtaani kwa niaba yetu,hivyo maandamano yetu
yamefanikiwa na watanzania wamepata ujumbe tuliotaka uwafikie kuwa tunapinga
matokeo ya uchaguzi mkuu 2015 yaliyotangazwa na tume ya taifa ya uchaguzi”,amefafanua
Kitalama.
Amesema
tangu Novemba 02,2015 hadi Novemba 03,2015 misururu ya magari ya polisi
yakiwemo ya maji ya kuwasha yakiwa na askari polisi yamekuwa yakiranda
randa mtaani hivyo hiyo ni ishara tosha kuwa polisi wanaandamana badala ya Chadema.
Hata hivyo kitendo cha Chadema kusitisha maandamano yao
katika wilaya ya Shinyanga kumepongezwa na baadhi ya wananchi kwa madai kuwa
kungesababisha uvunjifu wa amani huku wakishauri kuwa kama kweli Chadema
hajaridhishwa na matokeo hayo basi wasiruhusu hata wabunge wao kuapishwa.
Kwa upande wao baadhi ya wakazi wa Shinyanga wamesema ni
vyema serikali ingewaruhusu wafuasi wa Chadema
waandamane ili kueleza hisia zao juu ya matokeo ya uchaguzi mkuu
uliopita kwani ni maandamano ya amani.
Kusitishwa kwa maandamano ya Chadema kumekuja siku moja tu
baada ya jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga kuzuia maandamano na mikutano yote
katika kipindi hiki hadi pale wabunge na rais mteule wa jamhuri ya muungano wa
Tanzania atakapoapishwa ili kuimarisha ulinzi na usalama katika nchi kwa
kuepuka vitendo vyote vinavyoweza kuleta uvunjifu wa amani.
Na Kadama Malunde-Malunde1 blog
SOMA HAPA TAARIFA YA JESHI LA POLISI KUZUIA MAANDAMANO YA CHADEMA
Social Plugin