Mfanyabiashara Yericko Nyerere amepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, akikabiliwa na mashitaka matano ya kutoa taarifa za uongo kupitia mtandao wa kijamii wa Facebook.
Nyerere
alifikishwa mahakamani hapo jana na kusomewa mashitaka na mawakili wa
Serikali, Simon Wankyo na Paul Kadushi mbele ya Hakimu Mfawidhi, Cyprian
Mkeha.
Anashitakiwa
chini ya Kifungu cha 16 cha Sheria ya Mtandao Namba 14 ya 2015. Nyerere
anadaiwa Oktoba 25, mwaka huu katika eneo lisilojulikana, alichapisha
taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook, akidai kuwa “Piga
kura leo huku ukikumbuka kifo cha Mwangosi, Mateso ya Ulimboka na
Kibanda, mateso ya vijana wetu wa JKT, ukikumbuka hayo fanya uamuzi
sahihi bila ushabiki”.
Wanyo
alidai kuwa Oktoba 24, mwaka huu jijini Dar es Salaam, Nyerere
alichapisha taarifa za upotoshaji kupitia mtandao wa Facebook kuwa Taifa
la Tanzania kuanzia leo halihitaji amani, linahitaji haki tu.
Inadaiwa, alichapisha taarifa za uongo kupitia mtandao huo kuwa, “siku
ya leo mpaka siku ya kuapishwa Lowassa, taifa halihitaji amani, bali
taifa hili linahitaji haki tu, amani ilishatoweka siku nyingi,
kilichobaki ni uvumilivu tu…, njia sahihi ya kulitibu taifa hili ni kwa
dola dhalimu kutenda haki hata kama itawauma”.
Inadaiwa Nyerere aliendelea kudai kuwa “Uchaguzi
huu ni vita, anayedhani ni demokrasia apimwe akili…hii ni vita kati ya
umma na dola, ni vita kati ya wema na ubaya, kati ya shibe na njaa, kati
ya masikini na matajiri… umma umekosa amani na furaha, fursa pekee
waliyoipata watanzania wanamjua rais wao wanayekwenda kumchagua kesho,
jaribio lolote litakalofanywa na CCM na vibaraka wao la kukwamisha
matakwa ya umma, litaondoa hata ule uvumilivu kidogo walionao watanzania
na kisha vitazaliwa vichaa chongo ambavyo hata risasi na mabomu
hayatakizima”.
Aidha, anadaiwa siku hiyo hiyo alichapisha taarifa nyingine ya upotoshaji kupitia mtandao ikisema “mipango
ya hujuma ya JK toka Ngurdoto Arusha muda huu…Kikwete yupo Ngurdoto
Arusha na wakuu wote wa mikoa na wilaya Tanzania nzima pia wakuu wa
vyombo vya dola na wanadhimu mbalimbali… wakuu wa mkoa wanaelezwa kuwa
NEC kwa kushirikiana na CCM tayari wameshatengeneza kura bandia kwa
kutumia mfumo wa kalamu za kichina… pia wanaamuliwa kuhakikisha
wanahujumu kampeni za Ukawa kwa kutumia vyombo vya dola, wanaagizwa
kuhakikisha kamatakamata ya vijana bodaboda wiki moja kabla ya uchaguzi
na zaidi wanaagizwa wakawaagize maDC kote nchini kuhakikisha wanalinda
maslahi ya CCM siku yaUchaguzi."
Katika
mashitaka mengine, Nyerere anadaiwa Septemba 3, mwakahuu katika eneo
lisilojulikana alichapisha taarifa za uongo kuhusu uwepo wa akaunti ya
benki ya kughushi inayomilikiwa na mtanzania katika benki ya HSBC Tawi
la North London, ikionesha CCM imemwekea Dk Wilbrod Slaa Euro milioni
1.5 kupitia kwa mchumba wake, Josephine Mshumbusi ikiwa ni rushwa ili
kushinda uchaguzi mwaka huu.
Nyerere
anadaiwa alichapisha na kusambaza taarifa hizo za uongo kupitia mtandao
wa Facebook kwa lengo la kupotosha umma katika Uchaguzi mkuu wa mwaka
huu. Mshitakiwa alikana mashitaka na upande wa jamhuri ulidai upelelezi
wa kesi hiyo bado haujakamilika, pia hawana pingamizi la dhamana kwa
mshitakiwa huyo.
Nyerere aliachiwa kwa dhamana baada ya kutimiza masharti ya kuwa na mdhamini mmoja, aliyesaini hati ya Sh milioni tano. Kesi itatajwa tena Desemba Mosi mwaka huu.
Via>>>Mpekuzi blog
Social Plugin