Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

RAIS KIKWETE AFUNGUKA KUHUSU TANESCO….AMETOA AGIZO HILI




Rais Jakaya Kikwete, akipata ufafanuzi kutoka kwa Meneja wa Mitambo ya Kufua Umeme wa Gesi Kinyerezi jijini Dar es Salaam, John Mageni, wakati wa uzinduzi jana.





Rais Jakaya Kikwete, ameliagiza Shirika la Umeme nchini (Tanesco), kutumia fursa ya vyanzo vya kufua umeme ili kuuza nishati hiyo nchi jirani.

Aidha, Rais Kikwete ameahidi kuwa kufikia mwishoni mwa mwezi ujao, tatizo la umeme linaloikabili Taifa sasa litakuwa limepatiwa ufumbuzi kutokana na kukamilika kwa mradi wa mtambo wa umeme wa gesi wa Kinyerezi 1 jijini Dar es Salaam.

Rais Kikwete alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana alipozindua mtambo huo uliogharimu Dola za milioni 183 za Marekani (sawa na Sh. bilioni 400).

Kwa mujibu wa Rais Kikwete, mtambo huo uliowashwa jana na kuanza kufua umeme wa megawati 35, unatarajiwa kuongeza uzalishaji wake mara ya mbili ya sasa, kufikia megawati 70 ifikapo tarehe 20 mwezi huu, sehemu nyingine ya mtambo huo utakapoanza kufanya kazi.

“Kuongeza kasi ya kutumia vyanzo vyetu kuzalisha umeme nchini, itatupa fursa sisi Watanzania kuuza umeme kwa nchi jirani... changamkieni biashara hiyo nzuri maana wenyewe watakuwa na malipo ya uhakika badala ya kusubiri soko la ndani,” alisema Rais Kikwete.

Alisema serikali yake na itakayokuja, ina mpango mkubwa wa kuinua fursa za maendeleo kwa kuwekeza katika shughuli za kijamii nchini.

Alisema alipoingia madarakani mwaka 2005, alianza kazi nchi ikiwa na mgawo wa umeme na hata sasa anamaliza muda wake wa uongozi nchi ikiwa kwenye hali hiyo kutokana na ongezeko la majengo makubwa na viwanda vingi.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Ngosi Mwihava, alisema kuzinduliwa kwa kituo hicho kunafanya idadi ya vituo vya kufua umeme vilivyoanzishwa katika uongozi wa Rais Kikwete kufikia sita.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Felichesmi Mramba, alisema kwa sasa mtambo wa megawati 35 umeshawashwa na kuanza kusambaza umeme jijini Dar es Salaam na Oktoba 20, mwaka huu utawashwa mtambo mwingine wa kiasi kama hicho cha megawati na kufikia 70 na mwishoni mwa Novemba, utawashwa wa kuzalisha megawati 80 na kufanya jumla ya megawati 150 kutoka Kinyerezi 1.

Mramba akizungumzia tuhuma mbalimbali zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii kwamba mitambo iliyofungwa katika mradi huo ni chakavu na ya zamani, alisema siyo za kweli zina nia ya kuupotosha umma.

“Wale wanaosema mitambo hii ni chakavu na tunawapiga wananchi changa la macho, wajipange upya. Mitambo hii ni mipya na haijachakachuliwa hata kidogo Mheshimiwa Rais,” alisisitiza Mramba.

Alisema mitambo hiyo imetengenezwa nchini Marekani na kampuni inayoongoza kimataifa kwenye teknolojia hiyo.

Aidha, alisema Tanesco haina lengo la kuhujumu wateja wake na hali ya kukosekana maji kwenye mabwawa yanayozalisha umeme nchini inachangia kwa asilimia kubwa kutokea kwa mgawo wa nishati hiyo nchini.


CHANZO: NIPASHE

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com