Breaking News!! MWENYEKITI WA CCM MKOA WA ARUSHA NA KATIBU MWENEZI WAKE WAVURUGWA,WAIPIGA CHINI CCM NA KUHAMIA CHADEMA



Kushoto ni Katibu mwenezi wa CCM Arusha Isack Joseph akifuatiwa na mwenyekiti wa CCM mkoa wa Arusha Onesmo Nangole(mwenye suti)


Chama cha Mapinduzi (CCM) kimezidi kupata mtikisiko baada ya viongozi wa ngazi ya mkoa na makundi mbalimbali ya wanachama kukihama na kujiunga na upinzani.


Leo, ilikuwa zamu ya Mwenyekiti wa Mkoa wa Arusha, Onesmo Ole Nangole na Katibu wa Uenezi na Itikadi wa CCM mkoa huo, Isack Joseph waliojiondoa huku wakieleza wazi kuwa wanamfuata Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa.


Ole Nangole anakuwa mwenyekiti wa pili wa chama hicho katika ngazi ya mkoa kuhama akitanguliwa na Mgana Msindai.


Pia, hatua hiyo imekuja baada ya juzi, wanachama zaidi ya 200 wa Kata ya Engaruka, Monduli kudaiwa kuchoma kadi za CCM na kujiunga na Chadema akiwamo diwani wa kata hiyo na Mwenyekiti wa Kijiji cha Engarudika.


Wakizungumza na waandishi wa habari jana, viongozi hao walisema wameondoka CCM baada ya kutoridhishwa na mwenendo wa chama hicho hasa kwenye mchakato wa kumteua mgombea wa urais wa CCM.


Baada ya kutoa tamko lao, viongozi hao kwa pamoja na kwa mara ya kwanza walitoa salamu ya chama chao kipya ya “Peopleees” na kuitikiwa “Pooower”, huku Joseph akimaliza kwa kusema: “Mengine tutajifunza mbele ya safari.”


Ole Nangole ambaye ameshika wadhifa huo kwa miaka saba, alisema CCM ambayo alikuwa kiongozi tangu mwaka 1977 siyo ya sasa, akisema imetekwa na watu wachache wenye masilahi yao.


“Hiki chama kimetekwa na watu wachache, ambao wanavunja katiba na taratibu, nimeona sina sababu ya kubaki CCM kuanzia leo (jana) natangaza rasmi kukihama chama hiki nilichokitumikia kwa zaidi ya miaka 35,” alisema.


Alisema mchakato wa kupata mgombea wa urais wa CCM, ulitekwa na kikundi cha watu wachache ambao walikwenda na majina yao mifukoni, kwenye kikao cha kamati kuu hivyo, kutowatendea haki wagombea wengine.


“Kibaya zaidi ambacho kimetufanya kuondoka CCM ni matusi ambayo yanaendelea kutolewa na baadhi ya viongozi dhidi ya wenzao, hasa Lowassa, bila kujali ni kiongozi mkubwa wa Taifa hili na amefanya mambo mengi ya maendeleo,” alisema.


Bila ya kutoa mifano, Ole Nangole alisema wanashangazwa na viongozi wa juu wa chama hicho kuwapa vyeo vijana ambao wanawatukana viongozi, jambo ambalo halivumiliki.


“Tumeamua kuungana na Lowassa Ukawa kwa kuamini hakutendewa haki yeye na wanaCCM wengine ambao majina yao yalikatwa kinyume cha taratibu na sasa wanatukanwa,” alisema.


Alisema, Lowassa ameumizwa kwa kiasi kikubwa na wanaCCM wenzake na ametukanwa kwa tuhuma ambazo hazina ukweli wowote.


Kabla ya kuwa mwenyekiti wa mkoa, Ole Nangole alikuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Monduli kwa miaka 10, Diwani wa Longido na pia ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM tangu mwaka 1977.


Katibu wa uenezi


Akizungumza sababu ya kuondoka CCM, Joseph ambaye pia alikuwa ni Diwani wa Kata ya Monduli Mjini na alipita bila kupingwa katika kura za maoni ndani ya CCM hivi karibuni, alisema ameamua kujiondoa kutokana na demokrasia kumezwa na wachache.


“CCM sasa ni mali ya watu wachache, nimeamua kuacha nyadhifa zangu zote na kujiunga na Chadema ingawa nilipita bila kupingwa katika udiwani Kata ya Monduli mjini,” alisema.


Alisema ametafakari kwa muda mrefu kuhusu mustakabali wake ndani ya CCM na ameona hana sababu ya kubaki katika chama hicho akibainisha kuwa sababu ni kukiukwa kwa kanuni na taratibu zake ambazo zinahodhiwa na watu wachache.


“Kikubwa kilichonifanya kuipinga CCM ni kuona chama kinavunja taratibu na kanuni zake waziwazi, Kamati ya Maadili ya CCM haikuwa na mamlaka ya kukata majina ya wagombea lakini imefanya hivyo na kuondoa baadhi ya majina likiwamo la Lowassa,” alisema.


Alisema Lowassa ndiye aliyekuwa mfano wake wa kujifunza katika siasa, hivyo kwa jinsi alivyotendewa ameona hana sababu ya kubaki CCM kwani chama kimetekwa na watu wachache.


Amlaumu Kinana


Joseph alitumia fursa hiyo kukemea kauli ya hivi karibuni ya Katibu Mkuu wa CCM, Abdulrahman Kinana kuwa wagombea waliokatwa majina na kukimbilia upinzani ni makapi, akisema kauli hiyo imemkera zaidi akisema kwa historia ya Taifa, Lowassa hawezi kuwa kapi.


“Lowassa ni Mtanzania halali amefanya mambo mengi kwa Taifa hili sambamba na viongozi wengine, mimi nadhani hastahili kuitwa kapi,” alisema.


Joseph amekuwa Diwani wa Monduli mjini kwa miaka 10 na ameshika nyadhifa mbalimbali ndani ya CCM katika Wilaya ya Monduli, kabla ya kuwa katibu wa uenezi na itikadi Mkoa wa Arusha.


Kumsindikiza Lowassa


Viongozi hao pamoja na madiwani na wengine waliojiondoa CCM hivi karibuni na kujiunga na Chadema, jana waliondoka Arusha kwa ndege kuelekea Dar es Salaam kumsindikiza Lowassa atakapokwenda kuchukua fomu za kuwania urais leo.


Viongozi hao wanatarajiwa kupokewa makao makuu ya Chadema leo baada ya Lowassa kuchukua fomu za kuwania urais kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).


Kauli ya Chadema


Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Arusha, Derick Magoma alisema chama hicho kimewapokea na kinawapa haki zote kama wanachama wengine.


“Hiki ni chama cha demokrasia, tunawapokea viongozi hawa leo na leoleo wanaanza kazi ya kuiondoa CCM madarakani, tunawapa hadhi sawa na wanachama wengine wa Chadema,” alisema.


Alisema Chadema itaendelea kuwapokea makada wa CCM na vyama vingine ili kujiunga na Ukawa katika kuhakikisha wanaiondoa madarakani chama tawala.


“Hatutafunga milango, tunawakaribisha wanaCCM wote wanaokerwa na chama chao ambacho hakina sifa ya kuendelea kushika Dola, waje Ukawa tulikomboe Taifa,” alisema.


‘Waache waondoke’


Akizungumzia hatua ya viongozi hao kuhama, Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Alphonce Kinamhala alisema CCM haiwezi kuwabembeleza wanachama ambao wanataka kuhama.


Alisema amepata taarifa za kujiondoa CCM kwa viongozi hao kupitia simu lakini chama hicho hakina pingamizi kwa kuwa waliingia wenyewe na hawakulazimishwa kubaki.


“Waache waondoke, CCM ina wanachama wengi, tutajaza nafasi zao baadaye na ni vyema wameondoka na tumejua hatukuwa nao pamoja, sasa tunabaki na wanaCCM ambao tupo pamoja,” alisema.


Wawili wahama Mbeya


Mbali na Arusha, Mwenyekiti mstaafu wa UVCCM mkoani Mbeya, Reginald Msomba pamoja na aliyeshindwa kura za maoni kusaka ubunge Jimbo la Kyela kupitia chama hicho, George Mwakalinga wamejiunga Chadema.


Msomba, baada ya kukabidhiwa kadi ya Chadema na Mwenyekiti wa Chadema Mkoa wa Mbeya, Joseph Mwachembe alisema ameondoka CCM baada ya kuiona imepoteza mwelekeo na dhamira ya kuwatumikia wananchi.


“Hivi sasa kuna ubinafsi mkubwa ndani ya CCM na siyo chama kile nilichokuwa nakifahamu, chama ambacho kilikuwa na mtazamo wa kuleta maendeleo kwa wananchi,” alisema Msomba.


Mwakalinga alisema hivi sasa CCM imebaki kuwa ni ya kubeba watu wenye fedha, lakini si kwa dhamira ya dhati ya kuwakomboa Watanzania kama ilivyokuwa enzi za Mwalimu Nyerere.


Kibaha watishia


Wakati hayo yakitokea, kundi la wanachama zaidi ya 100 wa CCM wilayani Kibaha limetishia kujiondoa katika chama hicho na kuhamia Ukawa endapo Kamati ya Siasa ya Mkoa wa Pwani itaendelea kuwakingia kifua baadhi ya wagombea wanaolalamikiwa kucheza rafu.


Wanachama hao wakiwa kwenye Ofisi ya Waandishi wa Habari Kibaha, walisema wameamua kuweka wazi hisia zao kutokana na kamati ya siasa kukwepa kupitia rufaa za kupinga ushindi wa Silvestry Koka katika nafasi ya ubunge.


Mmoja wao ambaye ni mkazi wa Tamco, Paschal Ernest alisema kamati ya siasa ya mkoa imekwepa kupitia rufaa zilizowasilishwa tangu Agosti 4.


Kiongozi wa kundi hilo, Salum Ibadi alisema: “Tunaomba vyombo vya habari vitusaidie kutufikishia kilio hiki kwa Katibu mkuu wetu wa CCM na viongozi wengine wa kamati kuu wajue wapo wenzao wanakiharibu chama kwa mtindo huu.”


Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani, Mwinshehe Mlao alipoulizwa kuhusu madai hayo, alisema kwa kawaida rufaa inaanzia katika ofisi ya jimbo husika, inajadiliwa na wajumbe na kutoa mapendekezo yao.


Kuhusu kamati ya siasa kukwepa rufaa, Mlao alisema hakuna rufaa iliyowasilishwa mkoani ikakosa kujadiliwa labda kama haijafikishwa.


“Ni kweli Agosti 5 kalikaa kikao cha kamati ya siasa cha mkoa kiujadili majina ya wagombea lakini katibu wangu hakuniambia kama kuna rufaa hiyo,” alisema.


Mapema mwezi huu, wagombea wanne wa ubunge kupitia CCM, walikata rufaa kupinga ushindi wa Koka katika kura za maoni.
Imeandikwa na Mussa Juma, Julieth Ngarabali na Godfrey Kahango.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post