Noma Sana!! MSEKWA AMPASUA KINGUNGE NGOMBALE MWIRU


Makamu mwenyekiti mstaafu wa CCM, Pius Msekwa amemrushia kombora kada mkongwe wa chama hicho, Kingunge Ngombale-Mwiru kuwa, hazijui vyema kanuni zinazoongoza mchakato wa uteuzi wa mgombea urais kwa tiketi ya chama hicho tawala.


Huku akinukuu Kanuni za Usalama na Maadili, toleo la mwaka 2012, Msekwa alisema ilitumika ili kupambana na siasa zinazoendeshwa kwa nguvu ya fedha na kuwachuja wagombea ili kupata walio waadilifu.


Kauli ya Msekwa ni mwendelezo wa madai ya Kingunge aliyeitupia lawama CCM kuwa haikutenda haki katika mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM. Katika mchakato huo, Dk John Magufuli alichaguliwa kuwa mgombea urais akiwashinda Asha-Rose Migiro na Balozi Amina Salum Ali.


Kingunge aliyejitoa kindakindaki kumpigania Mbunge wa Monduli na Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, amekuwa akitoa matamko mbalimbali kuhusiana na mchakato huo na zaidi akisema haukutenda haki.


Amekuwa akikaririwa akisema wagombea wote 38 waliojitokeza walitakiwa kuhojiwa na Kamati Kuu, kisha wachujwe na kubaki watano na kupinga kitendo cha Kamati ya Usalama na Maadili kufanya kazi ya kuwachuja wagombea.


Msekwa ni mmoja wa viongozi wa zamani waliotoa mapendekezo yaliyokuwa msingi wa CCM kupata mgombea wake wa urais katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25 mwaka huu


Akizungumza na mwandishi wetu jana, Msekwa alinukuu vifungu vinavyoeleza majukumu ya Kamati ya Usalama na Maadili na chama hicho, kusisitiza kuwa wanaolalamikia mchakato huo, ama hawajazipitia kanuni hizo au hawazijui.


“Mzee Ngombale amezua madai kwamba eti mchakato wa kumpata mgombea urais wa CCM ulikuwa ni batili, kwa sababu eti ulikiuka kanuni za chama. Madai hayo yamepotosha kabisa ukweli wa jambo hilo. Kwani ukweli wenyewe ni kwamba kanuni za CCM zinazohusika zilifuatwa kwa ukamilifu. Kanuni hizo zilizotumika zinaitwa Kanuni za Usalama na Maadili, toleo la mwaka 2012. Pengine tatizo la mzee huyo ni kwamba hajazipata vizuri.”


Alisema: “Kwa mujibu wa Kanuni namba 3(3)(vii); Kamati ya Usalama na Maadili itachambua kwa makini ubora wa wanachama wanaoomba uongozi, kabla vikao vinavyohusika havijatoa idhini ya kuwaruhusu wateuliwe kugombea uongozi wanaouomba.”


“Kanuni hii ndiyo inaipatia uwezo Kamati ya Usalama na Maadili kufanya uchambuzi wa maadili ya wagombea wote kabla majina yao hayajapelekwa kwenye vikao ninavyofuata vya Kamati Kuu na Halmashauri Kuu ya Taifa.”


Alisema utaratibu uliowekwa na kanuni hiyo ulifuatwa kwa ukamilifu, kusisitiza kuwa haukuwa batili kama inavyodaiwa.


Akizungumzia lengo la kutoa kipaumbele cha kwanza kwa suala la maadili ya viongozi alisema: “Ni vyema ieleweke kwamba kanuni hii ilikusudiwa kupambana na ukosefu wa maadili ya viongozi ambao ni wanachama wa CCM na hususan kupambana na tatizo kubwa la ujio wa money-driven politics (siasa zinazoendeshwa kwa nguvu ya fedha).”


Alisema tatizo la siasa zinazoendeshwa kwa fedha lilijitokeza kwa nguvu wakati wa mchakato wa kuwania urais katika uchaguzi wa mwaka huu.

Via>>Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post