ACT- WAZALENDO : HATUJIUNGI NA UKAWA NG'OO!!

Kiongozi wa ACT – Wazalendo, Zitto Kabwe (pichani) amesema kuwa chama chake hakitashirikiana na vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), badala yake kitasimama chenyewe kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 25.


Kauli hiyo inazima minong’ono iliyotawala miongoni mwa wanachama wa ACT-Wazalendo waliokuwa wakimuuliza Zitto kuhusu chama hicho kujiunga na Ukawa.


Zitto alimaliza uvumi huo jana jijini Dar es salaam katika mkutano na viongozi wa chama, wanachama na watiania wa nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu.


Alisema ACT-Wazalendo haiwezi kuungana na Ukawa inayoundwa na vyama vya Chadema, CUF, NCCR-Mageuzi na NLD kwa vile sera ya chama hicho tofauti na vyama hivyo.


“Nawaomba niwatoe hofu, Chama cha ACT-Wazalendo kitasimama chenyewe kama kilivyo, hatutaki ushirikiano,” alisema Kabwe na kuongeza:


“Najua chama chetu bado ni kichanga, kina miezi mitano tangu kuanzishwa kwake, lakini si mnajua Timu ya Soka ya Mbeya City?” aliwauliza wajumbe waliojibu: “ndiyo.”


“Ile timu ilianza kama masihara, lakini mwisho wa siku ikawa tishio kwa timu za Ligi Kuu, basi chama hiki kitakuwa hivyo,” alisema Zitto na kushangiliwa na wajumbe waliohudhuria mkutano huo.”


Alibainisha kuwa chama chake kimedhamiria kuwatumikia Watanzania na kushika dola kwa njia halali.


Alisema ACT – Wazalendo kina azimio la Tabora, ambalo ndani yake kuna kipengele namba nne, kinachozungumzia miiko na mali za viongozi kabla ya kujiunga na chama hicho na kwamba chama chochote kitakachotaka kujiunga ACT, lazima kikubaliane na kipengele hicho ili kuzuia mianya ya rushwa na uroho wa madaraka ndani ya chama.


Aliwataka wanachama kutotishika na mtikisiko wa kisiasa utakaotokea muda wowote kuanzia wiki hii, kwani ni mambo ya kawaida.


“Mtikisiko huu usiwatie presha, mtulie tena mnyooshe miguu juu, huu ni upepo wa kisiasa na wala haututoi kwenye mstari. Narudia tena viongozi wangu ACT, mkoa msiyumbishwe na hali itakayojitokeza,” alisema.


“Hatuna presha kufanya vikao vya mara kwa mara, chama kwa masilahi ya watu fulani, tutafuata ratiba yetu vizuri,” alisema Zitto.


Alisema ACT-Wazalendo kinaendeshwa na wanachama na siyo viongozi, hivyo kila uamuzi hufuata kanuni na taratibu za chama.


“Ndiyo maana kuna chama kimoja (hakukitaja), hadi leo (jana) kinapiga danadana kumtangaza mgombea wake wa urais sijui wanamsubiri atoke kwenye Sayari ya Mars,” alihoji Zitto.


Zitto alisema kuwa atashirikiana na wagombea wote watakaopitishwa na chama hicho kugombea nafasi mbalimbali ili majimbo 10 ya Mkoa wa Dar es Salaam yaende ACT-Wazalendo.


“Juzi nilikuwa Jimbo la Kigoma Mjini, kuna chama kimoja kilikuwa kinatafuta mgombea atakayewakilisha jimbo hilo maana kila anayeambiwa anakataa, kwa sababu wanasema ni ngome ya ACT-Wazalendo,” alisema.

Na Bakari Kiango-Mwananchi

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com
Previous Post Next Post