Baadhi ya vifaa vilivyokamatwa msikitini na polisi ambapo watu 10
wanashikiliwa na jeshi hilo mjini Morogoro. Picha na Lilian Lucas
Watu 10 wanashikiliwa na polisi mkoani Morogoro baada ya
kukamatwa msikitini wakiwa na milipuko 30, sare za jeshi na bendera
nyeusi inayodaiwa kutumiwa na kundi la wapiganaji wa Al Shabaab wa
nchini Somalia.
Katika tukio hilo, mmoja anayesadikiwa kuhusiana
na watu hao waliokamatwa aliuawa na wananchi wenye hasira baada ya
kumjeruhi kwa panga askari polisi aliyekuwa akipambana naye.
Akizungumza na waandishi wa habari leo, Kamanda wa
polisi mkoani Morogoro, Leonald Paul alisema tukio hilo limetokea jana
(Aprili 14 mwaka huu) majira ya saa 3.30 usiku katika kitongoji cha
Nyandero, tarafa ya Kidatu wilayani Kilombero.
Kamanda Paul alimtaja mtu aliyefariki kuwa ni
Hamad Makwendo ambaye umri wake haujafahamika ambaye ni mkazi Manyasini
Ruaha wilayani Kilombero.
Aidha alisema siku ya tukio polisi walipata
taarifa kutoka kwa raia wema kuhusu watu hao na kwamba walitaarifiwa
kuwa wanajihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu na polisi waliamua
kufatilia nyendo zao.
Akisimulia tukio hilo, Kamanda Paul alisema:
“Polisi walipata taarifa kuwa watu hao walitumia usafiri wa bajaji mbili
kwenda kusikojulikana na wakati wakiendelea na zoezi la kufuatilia
ndipo walikutana na bajaji moja ikiwa na abiria mmoja ambaye ni Mkwendo
na kuisimamisha.”
Alisema kuwa bajaji hiyo iliposimama marehemu huyo
aliruka na kuanza kukimbia ndipo askari mwenye namba F .3323 Koplo
Nasoro alianza kumkimbiza na alipomkaribia mtuhumiwa huyo alichomoa
jambia alilokuwa nalo na kumkata askari huyo eneo la shingoni.
Askari mwingine mwenye namba E.9245 Koplo Chomola
ambaye alikuwa nyuma alifanikiwa kumpiga risasi ya mguu mtuhumiwa
huyo,ambapo alipoanguka chini wananchi wa eneo hilo tayari walifika
katika eneo hilo na kuanza kumshambulia marehemu huyo kisha kumchoma
moto kwa hasira.
Kamanda huyo alisema walianza kuwasaka watu wengine ambao walipata taarifa wapo katika Msikiti wa Suni uliopo Kidatu.
“Polisi walipofika katika msikiti huo waliuomba
uongozi wa msikiti huo kuwatoa watu wote waliokuwa msikitini ili kuweza
kubaini watu ambao wanatiliwa mashaka,”
Alisema polisi walendelea na ukaguzi na kuwakamata watu hao 10 wakiwa na vifaa hivyo na kuwatia nguvuni.
Kamanda huyo alitaja vitu vilivyokutwa katika
mabegi yaliyokuwa ndani ya msikiti huo ni pamoja na milipuko 30, bendera
nyeusi yenye maandishi ya Kiarabu yakisomeka ‘Mungu Mmoja’, majambia,
bisibisi, vinyago vya kuziba uso (masks), nguo za jeshi, misumeno ya
chuma na spana.
Via~~Mwananchi
Social Plugin