TAARIFA ZAIDI KUHUSU VURUGU ZA IRINGA,POLISI KUUA MWANANCHI,KITUO CHA POLISI KUCHOMWA MOTO

Kumetokea vurugu za aina yake katika eneo la Ilula mkoani Iringa kati ya askari polisi na wananchi baada ya mwanamke ambaye hajafahamika jina kufariki dunia wakati wa oparesheni maalum ya jeshi la polisi kukamata watu wanaouza na kunywa pombe ikiwemo pombe haramu aina ya gongo mida ya kazi.


Tukio limetokea  jana Februari 24,2015 saa sita mchana katika eneo la Ilula wilaya ya Kilolo mkoa wa Iringa

Habari kutoka eneo la tukio zinasema kuwa  polisi walipofika eneo hilo watu waliokuwa eneo hilo walianza kukimbia kuhofia kukamatwa ndipo polisi mmoja akamchota mtama mwanamke mmoja aliyekuwa anakimbia,akaanguka na kufariki dunia hapo hapo.

Kufuatia kifo hicho, wananchi walihamasishana na kuanza kupambana na askari hao huku wakiwa wamebeba silaha za jadi ikiwemo fimbo na mawe,wakazuia magari yaendayo mikoani,kuchoma matairi barabarani huku polisi nao wakirusha mabomu ya machozi kuwatawanya wananchi hao.

Inaelezwa kuwa wananchi hao mbali na kuharibu mali mbalimbali za polisi  ikiwemo kuchoma moto magari matatu ya polisi  kituo  Ilula na vitu vingine vingi.

Mwakilishi wa Malunde1 blog mkoani Iringa Yonna Mgaya  anayefanya kazi Radio Furaha ya Iringa amezungumza na kaimu kamanda wa polisi mkoa wa Iringa Pudensiana Protas ambapo kamanda huyo wa polisi amesema polisi walipata taarifa kuwa kuna uuzaji wa pombe za kienyeji ikiwemo pombe haramu aina ya gongo na walipofika pale watu wakaanza kukimbia hovyo.

Kamanda huyo wa polisi amesema wakati wananchi wakikimbia ovyo ndipo huyo  mwanamke akateleza  na kuanguka akafariki dunia.

Kamanda Protas mesema polisi wanaendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo na jina la mwanamke aliyefariki halijafahamika na kwamba watatoa taarifa rasmi juu ya tukio hapo baadaye.

Na Yonna Mgaya-Malunde1 blog Iringa

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527