KITUO CHA POLISI CHAVUNJWA KWA NGUVU HUKO GEITA

Jengo la Kituo cha polisi Nkome linavyoonekana nyuma ya Ng'ombe kabla ya kuvunjwa,picha iliyopigwa hivi karibuni wakati waandishi wakifuatilia sakata la mtendaji wa kata hiyo Francis Kagoma la kumwiba ng'ombe huyo(pichani) kabla ya kukamatwa na polisi kisha kufungwa nje ya kituo hicho baada ya mtendaji kutoroka -Picha na Victor Bariety Malunde1 blog Geita

Mkuu wa kituo cha polisi Nkome Gwaga Mtawa (aliyevaa tisheti ya misitari miekundu)katikati akiongea na waandishi wa habari na wananchi nje ya kituo cha polisi hivi karibuni kabla hakijavunjwa katika sakata la mtendaji kuiba ng'ombe pichani-Picha na Victor Bariety -Malunde1 blog Geita


Katika  hali isiyokuwa ya kawaida,jengo lililokuwa likitumika kama kituo kidogo cha polisi Nkome Tarafa ya Bugando Wilaya ya Geita limebomolewa na mmiliki wake ili polisi wa kituo watafute sehemu nyingine baada ya kutokea mvutano katika ulipaji wa kodi ya pango hilo.

Kufuatia hali hiyo,kwa sasa Mkuu wa kituo hicho Gwaga Mtawa pamoja na askari wake,hawana mahala pa kuishi wala sehemu ya kufanyia shughuli zao za kiofisi,baada ya kutimuliwa na mmiliki wa Nyumba hiyo kwa kubomoa jengo hilo walilokuwa wamelipanga kwa miaka mingi sasa kutokana na kushindwa kulipa kodi kwa kipindi cha miaka mitatu.

Hali hiyo inatokana na Mmiliki huyo,Siki Deusi Mkazi wa Katoro kubomoa sehemu ya  nyumba hiyo,baada ya kuonekana mwelekeo wa polisi kumlipa kushindikana.

Akizungumza na Malunde1 blog,Deusi alisema anadai kodi ya sh.3.3 Milioni za miaka mitatu na kwamba amechukua hatua  hiyo baada ya kuona askari wanatumia ubabe hasa wakati anapoenda kudai fedha hizo.

‘’Nimehangaika mno kudai kodi yangu…sijalipwa kila nikidai ni propaganda tu..kuna siku nilienda kudai wakasema wanakaa kikao na wafanyabiashara,lakini hawakunilipa.Na hata nilipowaomba wanilipe hata mwaka mmoja waendelee kukaa hakuna’’

‘Sasa nikiwadai wananitishia,wanasema na mimi ni miongoni mwa wafanyabiashara tunaolindwa na hao askari…nilipoendelea kuwadai wakasema niende mahakamani..kwa hiyo mimi sikutaka yote hayo hawezi kuishi kwenye nyumba yangu kibabe nimeamua kuivunja ili waondoke wakatafute sehemu nyingine’’alisema.

Alisema baada ya kuona anadanganywa kuhusu kulipwa ndipo Januari 20,mwaka huu aliamua kwenda kuvunja,uzio wa nyumba hiyo,bango la kutambulisha kituo cha polisi,choo na bafu na kuwapa notisi ya siku tatu wahame kwenye nyumba yake.

‘’Nilifanya kazi hiyo kwa hasira sana na sikutaka anisogelee mtu..nimeamua kuvunja ili atayeingia nitamjengea upya na kama watashindwa kutoka kwa siku hizo tatu naenda kung’oa bati,waondoke kabisa nimechoka kuvumilia’’alisema Deusi.

Alisema alichukua amzi huo baada ya kuona viongozi wa kijiji na kata hawana msaada kwake kutokana na aliyekuwa mtendaji wa kata hiyo kuhamishwa na mwenyekiti kumaliza muda wake ambao walisaini mkataba wa jengo hilo..

Mwenyekiti wa serikali ya kijiji hicho,Anjelo Daniel alisema fedha hizo zilikuwepo lakini zilitafunwa na viongozi wa kata hiyo akiwemo diwani wa kata,kitendo ambacho alidai ni kuwadhalilisha askari kwa kufukuzwa kutokana na kushindwa kulipa kodi.

Kwa upande wake,Diwani wa kata ya Nkome,Karema Chilatu ambaye ni miongoni wa viongozi waliokuwepo wakati wa kusaini mkataba huo alikiri jengo hilo kubolewa kutoka na kushindwa kulipa kodi kwa mmiliki huyo baada ya mapato ya kulipa kutopatikana.

‘’Askari wetu hao ambao wako watatu..tuliwaweka pale tangu mwaka 2008,kusubiri ujenzi wa kituo cha polisi ambacho kipo katika hatua ya kukamilika..Lakini Mmiliki wa nyumba hiyo alikubaliana na wafanyabiashara kwamba watamlipa..lakini imekuwa kimya na juzi..juzi alikuja kubomoa’’alisema na kuongeza.

‘’Askari wetu tumeamua kuwatafutia nyumba nyingine..wakute wanaishi pale,ujenzi wa kituo cha Polisi ukikamilika watahamia katika jengo lao..kwani walipokuwa pamevunjwa uzio,choo na vitu vingine na sisi hatuna namna ya kumlipa kwani mapato hakuna’’.

Kamanda wa polisi mkoani Geita,Joseph Konyo akizungumzia tukio hilo,alikiri jengo hilo kubomolewa na baada ya serikali ya kijiji kushindwa kulipa kodi kwa kipindi chote hicho.

‘’Suala hili linatokana na serikali ya kijiji kushindwa kulipa,kwani serikali hiyo ndiyo ilikuwa inawajibika kufanya hivyo..lakini tayari tumepata nyumba nyingine ambayo askari sasa wanaishi pale wakati ujenzi wa kituo ukiendelea’’.
Na Victor Bariety-Malunde1 blog Geita

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527