Serikali wilayani Kahama mkoani Shinyanga
kwa kushirikiana na mashirika mbalimbali imeshauriwa kuweka utaratibu wa
kufanya mikutano mara kwa mara ili kutoa elimu ya
Ukimwi hasa katika maeneo ya vijijini ambapo jamii bado
haijawa na uelewa wa kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.
Wakizungumza jana katika Tamasha la Siku
ya Ukimwi Duniani, Baadhi ya wananchi wa Kijiji cha Chapulwa Kata ya
Mwendakulima wamesema ipo haja ya serikali kufanya mikutano na
wananchi hali itakayowasaidia wananchi kujitambua na kufahamu njia za
kukabiliana na maambukizi ya VVU.
Baadhi ya wananchi hao, Diana Dotto na
Leonald Paul wameupongeza uongozi wa kampuni ya ACACIA kupitia mgodi
wa Buzwagi kwa kubuni mbinu hiyo ambayo imesaidia vijiji vinavyozunguka mgodi
huo kupata mwanga wa kutambua njia ya kujikinga na Ukimwi kwa njia
ya Hamasa za nyimbo na ujumbe wa viongozi mbalimbali.
Amesema elimu ya kupima ukimwi kwa hiari
katika maeneo ya vijijini bado ni duni ambapo hali hiyo inatokana na
kutokuwepo kwa elimu inatotolewa na viongozi na kwamba viongozi wa vijiji na
Kata wawe mstari wa mbele katika kubuni hamasa ya kuelimisha jamii.
Afisa mahusiano wa Mgodi wa ACACIA-
Buzwagi David Kilala amesema wameamua
kufanya mashindano ya kutafuta nyimbo bora yenye ujumbe mzuri wa
kupinga maambukizi, na unyanyapaa kwa watu wanaoishi na Ukimwi
ili kuishirikisha jamii katika kupata ujumbe wa Ukimwi.
Amesema pamoja na mambo mengine
zoezi hilo la kushirikisha jamii pamoja na kufanya matamasha ni endelevu kwa kata
ya Mwendakulima ambapo watatumia nafasi hiyo kuielimisha jamii mbinu
za kupunguza maambukizi ya Ukimwi pamoja na shughuli zingine za maendeleo.
Siku ya Ukimwi Duniani huadhimishwa
Desemba Mosi kila mwaka na maadhimisho ya siku hiyo katika Mkoa wa Shinyanga yafanyika
katika Kata ya Lunguya halmashauri ya Msalala wilayani Kahama.
Na Ndalike Sonda-Kahama