WANAWAKE WATAKIWA KUHIMIZA WAUME ZAO WAFANYIWE TOHARA KUJIKINGA NA UKIMWI


Wanawake wametajwa kuwa na nafasi kubwa ya kuwashauri pamoja na kuwahimiza waume zao na watoto wa kiume kufanyiwa tohara ikiwa ni njia moja wapo ya njia ya  kujikinga na maambukizi ya virusi vya Ukimwi.


Akizungumza  jana katika Kijiji cha Mwendakulima wakati wa tamasha la kutafuta  kikundi bora kitakachohamasisha siku ya Ukimwi duniani Mratibu wa Ukimwi wa halmashauri ya mji wa Kahama mkoani Shinyanga  Elibariki Minja aliwataka wanawake kutowaonea aibu waume zao badala yake wawaeleze.

Alisema kama wanawake watakuwa mstari wa mbele kuwashauri wanaume ambao hawajafanyiwa tohara itasaidia sana kupunguza maambukizi ya Ukimwi pamoja na  kuifanya jamii kuelimika kanda ya ziwa hususani Mkoa wa Shinyanga ambapo wanaume bado hawajawa na elimu ya kutosha kufanyiwa tohara.

“Ndugu zangu wanawake naomba muwasihi na kuwahimiza waume zenu ambao bado hawajapata tohara wapatiwe ili kujikinga na Ukimwi, pamoja na kuwapeleka watoto wa kiume kufanyiwa tohara”,aliongeza Minja.

Alisema kama wanaume watafanyiwa tohara itasaidia kuwapunguzia maambukizi ya virusi vya Ukimwi kwa asilimia 60 hivyo wanapaswa kuwahamasisha wananume ambao bado wanaona aibu ya kufanyiwa tohara.

Alisema  hospitali ya wilaya ya Kahama imetenga kitengo cha kufanyia tohara  kila siku hivyo  ni nafasi ya kila mwanamume ambaye bado hajafanyiwa kwenda kufanyiwa zoezi hilo ambalo linatolewa bure bila malipo.

Kwa upande wake  meneja Mahusiano wa Mgodi wa ACACIA Buzwagi Yunia Wangoya alisema mgodi bado unaendelea kujikita katika jamii inayowazunguka katika kushiriki kwenye shughuli za maendeleo pamoja na  kujumuika pamoja kwenye shughuli mbalimbali kama sera yao katika kuimarisha uhusiano na jamii inayowazunguka.

Na Ndalike Sonda-Kahama

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527