HATARIII_ MAJAMBAZI YAUAWA KWA KUPIGWA MAWE KISHA KUTUMBUKIZWA MTONI HUKO TARIME

Watu watano wanaosadikiwa kuwa majambazi, wamepigwa kwa mawe hadi kufa wakijaribu kutoroka nguvu za umma kwa kutumia Mto Mara, wilayani Tarime huku wakiwa na bunduki mbili zinazotumika vitani aina ya sub machine gun (SMG). 



Tukio hilo lilithibitishwa na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Lazaro Mambosasa. 



Kamanda Mambosasa alisema watu waliouawa katika tukio hilo la juzi mchana hawajafahamika kwa majina wala uraia wao. 



Hata hivyo alisema siku ya tukio, majambazi hao wakiwa na silaha za kivita, walionekana wamejificha vichaka karibu na makazi ya wananchi wa kitongoji cha Nyabirongo, kijiji cha Gibaso katika Kata ya Nyarukoba, Tarafa ya Ingwe iliyopo jirani na hifadhi ya Serengeti. 



Lakini baada ya kushitukiwa, walizingirwa na wananchi wenye silaha za jadi zikiwemo mawe, marungu na mapanga huku wakipiga mayowe ambapo majambazi hao walijibu kwa kurusha risasi hovyo ili wananchi wasiwakaribie. 



Wakati wakirusha risasi hizo zilimjeruhi mwananchi mmoja, Kagore Paul begani, na kuwaongezea hasira wananchi walioendelea kuwasakama katika eneo walilojificha. 



Mayowe waliyopiga yaliwaleta watu wengi zaidi muda ulivyokuwa unakwenda kiasi cha majambazi hao kuzidiwa na  kuamua kukimbia kwa kupitia Mto Mara, ili waende upande wa pili wa wilaya ya Serengeti. 



Kamanda anasema: "Wakazi wa kijiji hicho na vijiji jirani walijitokeza kwa wingi kwani ilikuwa mchana na kupambana na watu hao huku wakikimbilia mto Mara kutaka kuvuka mto huo  kwenda  wilaya ya Serengeti kuingia mbugani, lakini juhudi zao za kutaka kuvuka hazikifanikiwa. 



“Wananchi wa vijiji vya upande wa pili Wilaya ya Serengeti nao walijitokeza na kuziba njia hali iliyowalazimu watuhumiwa kuingia mtoni na kutaka kuogelea huku wakitupa silaha walizokuwa nazo majini  na hapo ndipo walipopigwa mawe na marungu wakiwa majini na kufa. 



“Jeshi letu la Polisi lilifika na kusaidia kuopoa miili ya watu hao watano ambapo mmoja alikutwa na risasi 11 mfukoni na mwingine alikutwa na risasi nne na fedha za Kenya Sh 350 (sawa na fedha za Tanzania sh 7,000) ambapo inasadikiwa huenda watuhumiwa wakawa raia wa nchi jirani ya Kenya.” 



Kwa sasa, miili ya watu hao imehifadhiwa katika chumba cha maiti cha Hospitali ya Wilaya Tarime huku jeshi la polisi likiendelea na uchunguzi juu ya tukio hilo. 



Naye Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Tarime, Dk Bernard Makonyu amethibitisha kupokea miili ya watu watano iliyofikishwa hospitali hapo na gari la polisi huku matumbo ya marehemu yakionekana kuvimba kutokana na kunywa maji mengi kabla ya kufikwa na mauti. 



Hilo ni tukio la pili katika kipindi cha wiki tatu ambapo Agosti 3 mwaka huu watu wanne, wakiwemo raia watatu wa Kenya na Mtanzania mmoja waliuawa kutokana na matukio ya ujambazi katika kijiji cha Mriba.

TAFADHALI BOFYA HAPA U LIKE PAGE YETU TUKUTUMIE "HABARI" MOJA KWA MOJA KILA ZINAPOTOKEA

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527