Utata mtupu!!! KAULI YA MBUNGE WA CCM LEMBELI YA "CCM SI MAMA YANGU" YAWAPA PRESHA VIONGOZI WA CCM MKOA WA SHINYANGA

MBUNGE WA JIMBO LA KAHAMA JAMES LEMBELI

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Shinyanga kimeeleza kusikitishwa na kauli iliyotolewa na mwanachama wa chama hicho ambaye pia ni Mbunge wa Kahama, James Lembeli kwamba CCM si mama yake.


Wakizungumza na waandishi wa habari kwenye ofisi za Makao Makuu ya CCM, viongozi wa juu wa chama hicho wakiongozwa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja, viongozi hao walisema kauli hiyo ni ya kushtua.

 

“Chama Cha Mapinduzi Shinyanga kinalaani vikali kauli ya Lembeli aliyoitoa hivi karibuni na kunukuliwa na vyombo vya habari akisema ‘CCM si mama yangu’.

“CCM Shinyanga tumeshtushwa na kauli ya Lembeli anayetokana na CCM, kwani kauli hii hatukutegemea sote kama ingeweza kutolewa na mwanachama ambaye tena ni kiongozi ndani ya chama,” alisema Katibu wa Siasa na Uenezi wa Mkoa wa Shinyanga, Emmanuel Mlimandago.
Alisema CCM haina tatizo na msimamo wa Mbunge huyo kuhusu msimamo wake wa serikali moja, mbili, tatu, nne au serikali ya Tanganyika kwani huo ni uhuru wake binafsi; lakini tatizo ni kauli kuwa CCM si mama yake kwani ameitoa mahali ambapo si sahihi.

Katibu huyo wa Itikadi na Uenezi, alisema jambo la ajabu ni kwa Mbunge huyo kulitumia jina la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere vibaya kwa kujifananisha na kauli zake wakati akiwa hana hadhi na sifa za Mwalimu Nyerere.

“Kwa Lembeli kujifananisha na Baba wa Taifa ni matumizi mabaya ya kujitwisha sifa asizostahili kwani Mwalimu Nyerere alikuwa na karama, heshima na busara kubwa za pekee na aliheshimika duniani kote pia alikuwa anatoa kauli zake kutokana na mazingira yaliyokuwepo wakati husika,” alisema Mlimandago.

Kwa upande wake Mgeja, alisema pamoja na kuelezwa kukerwa na kauli hiyo, CCM itatumia vikao halali katika kujadili kauli hiyo ya Lembeli ili kuona hatua stahiki zinazoweza kuchukuliwa kulingana na uzito wa kauli yake hiyo.

Akizungumza kwa simu akiwa Kahama, Lembeli alisema hawezi kuwazuia viongozi hao wa CCM Mkoa wa Shinyanga kusema jambo wanalolitaka wao; kwa vile ni haki yao kutoa maoni yao kama ilivyokuwa haki yake na yeye kutoa maoni yake kwa jambo lolote.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post