TFDA YAPIGA MARUFUKU VIPODOZI 222,YADAIWA VINA VIAMBATA VYENYE SUMU

MAMLAKA ya Chakula na Dawa (TFDA) imepiga marufuku vipodozi 222, baada ya kugundulika kuwa vina viambata vyenye sumu.


Hayo yamebainishwa na Kaimu Meneja wa TFDA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Rodney Alananga.


Analanga alisema kuwa vipodozi hivyo vimepigwa marufuku baada ya kufanyika kwa uchunguzi wa kimaabara ambapo uchunguzi huo umegundua kuwepo kwa viambata 11 vyenye sumu vinavyoweza kusababisha madhara kwa binadamu.


“Mpaka sasa tuna viambata 11 vya kisayansi ambavyo tumevichunguza na kugundua kuwa vina madhara kwa mtumiaji. Tumegundua karibu vipodozi 222  nchini vina viambata hivyo,’’ alisema.


Alisema kutokana na hali hiyo TFDA inadhibiti uingizwaji na usambazaji wa vipodozi hususan kwenye mipaka rasmi kwa kuweka mawakala wa mamlaka hiyo kwa ajili ya kupima vipodozi vinavyoingizwa kwenye mipaka hiyo.


Alisema kuwa moja ya vipodozi vyenye sumu ambavyo ni changamoto kuvidhibiti ni mafuta ya Carolite ambayo hutumiwa na watu wengi licha ya kuwa na madhara ambayo ni ya muda mfupi na mrefu.


Aliyataja madhara ya muda mfupi yanayotokana na kipodozi hicho ni muwasho, kutokea kwa mabaka meusi ambapo madhara ya muda mrefu ni kansa ya ngozi ambayo hutokea baada ya sumu kujikusanya taratibu. 

Madhara mengine ni watoto kuzaliwa wakiwa na mtindio wa ubongo.


Analanga alitoa wito kwa wananchi na wafanyabiashara wanaouza na kuagiza vipodozi salama pamoja na kuonana na wataalamu wa TFDA ili kuhakiki vipodozi hivyo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post