MITAZAMO TOFAUTI KUHUSU MAADHIMISHO YA MIAKA 50 YA MUUNGANO WA TANGANYIKA NA ZANZIBAR ULIOZAA TANZANIA


Dar/ Mikoani.  Wakati leo ni maadhimisho ya  miaka 50 ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar uliozaa taifa la Tanzania, wasomi, viongozi wa dini, watendaji wa Serikali na wananchi wa kawaida wamekuwa na mitazamo tofauti kuhusu uhai wa Muungano huo.
Wakizungumza na gazeti hili kwa nyakati tofauti, baadhi walitaka Muungano huo uvunjike kwa madai ya kutokuwa na manufaa yoyote, au uwe wa Serikali moja, huku wengine wakitaka uenziwe kwa sababu ndiyo chachu ya amani, umoja na mshikamano uliopo sasa.
Moshi
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha St. Augustine, Padri Francis Shawa alisema: “Muungano uendelee ila kuwe na serikali moja kama ilivyokuwa awali na Rais akitoka Zanzibar makamu atoke Bara na kusiwe na marais wawili.”
Alisema  wadhifa wa Rais wa Zanzibar na makamu wake viondolewe na pande zote zikubali baadhi ya vitu kutoa sadaka kwa kuvipoteza.
“Nakerwa  zaidi na Zanzibar kuwa na Katiba yao , wakati Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inasema Zanzibar ni sehemu ya nchi yake pia. Wakati wa Sherehe za Muungano, Rais wa Zanzibar ndiye anaonekana mwenye nguvu, kitu ambacho siyo sahihi. Rais wa Tanzania ndiye apewe hadhi kubwa,” alisema.
Diwani wa Kata ya Kilema Kusini, Kawawa Lubega alipendekeza Serikali mbili na alitoa sababu kuwa hata Serikali mbili za sasa bado wananchi hawajazifahamu vizuri. Lubega alisema kwamba shirikisho la serikali tatu litasababisha Rais atakayekuwapo madarakani akose nguvu kiuchumi na kiutawala.
Ofisa Elimu wa Shule za Sekondari za Wilaya ya Moshi, George Jidamva alipendekeza kuwapo kwa serikali mbili, lakini akashauri Katiba zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar, ziwekwe mezani ili dosari zilizopo zirekebishwe akitaja kipengele cha madaraka ya Rais.
Mwanasheria wa Serikali, Wilaya ya Moshi, Glorian Issagya alipendekeza pia serikali mbili ziendelee, lakini akasema wabunge waliojitoa bungeni, warudi ili changamoto zinazojitokeza ziweze kufanyiwa kazi zisije zikaleta athari hapo mbeleni.
Kuhusu mchakato wa Katiba Mpya, mwanasheria huyo alipendekeza ungepitia kwenye Halmashari za Wilaya na hali hiyo ingekuwa rahisi kwa kila mtu kutoa maoni yake kwani atakuwa amepata elimu kupitia vitongoji, vijiji hadi kata.
Songea
Naye mwanasiasa, Asha Kitambuli mkazi wa Wilaya ya Tunduru alisema kuwa binafsi anapenda Muungano uendelee kuwapo akieleza kuwa una faida nyingi na kwamba  wanaopenda uvunjike ni waroho wa madaraka na wabinafsi, akataka waache kuvuruga Muungano.
Aliongeza kuwa, Muungano uendelee kwani ndiyo umetufikisha tulipo na kwamba hapendi uvunjike bali kero zilizopo zirekebishwe ikiwa  ni pamoja na Watanzania Bara wawapo Zanzibar kupewa uhuru wa kufanya biashara kama ilivyo kwa Wazanzibari.
Naye Anispheta Malingali, mkazi wa Songea alisema Muungano uvunjwe akidai kuwa hauna faida kwa Watanzania Bara, aliosema wamekuwa wakinyenyekea Wazanzibar bila mafanikio na wenzao bado hawatambui mchango wa Muungano huo zaidi ya kulalamika kila kukicha.
“Mimi binafsi naona bora tuuvunje huo Muungano, sioni faida yake kwani wenzetu ndiyo wanafaidi kutoka kwetu. Sisi hatuna hata raha ya Muungano, kila kukicha wenzetu wanadai huduma muhimu kama afya, maji na umeme na wanatekelezewa, lakini bado hawaoni faida, wamepewa hadi Bunge lao bado hawajaridhika, wamepewa Serikali bado hawaridhiki. Binafsi sioni haja ya kuendelea kuungana na watu walalamishi wanaopenda machafuko,”alisema Malingali.
Mtwara
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo cha Stella Maris, mkoani Mtwara, Dk Aidan Msafiri, alisema kuwa dhana ya Muungano ni nzuri kwani umoja ni nguvu na Muungano ni kama mwili wa binadamu. Kikubwa ni kuzingatia maadili ya kuungana ni lazima wote walioungana kushirikiana, kuwe na uwazi, haki  na usawa.
Yaani walioungana wawe kama wanandoa, pia kuwe na faida kwa wote walioungana na tujifunze kwa wenzetu walioungana mfano Marekani.
Alisema kwamba kusiwe na ubabe wa kulazimisha serikali mbili au tatu, lakini ni vyema tukarudi kwenye serikali moja. Kuwa na serikali mbili au tatu kutakuwa na changamoto kubwa, tuwe kitu kimoja.
Naye Katibu Mtendaji wa asasi ya kiraia ya Faidika Wote Pamoja (Fawopa) la mkoani Mtwara, Komba Baltazary alisema: “Muungano una faida kubwa kwani tumechanganya nguvu za Wabara na Wazanzibari, hivyo kuwe na mfumo bora wa uchumi.”
Aliongeza katika muundo kwa maana ya kubakia kwa Tanganyika na Zanzibar kuwe na utambulisho kwa kila nchi kati ya nchi hizo.
“Tuwe na muundo unaoweza kujadiliwa na wananchi wote kama yalivyotolewa maoni kwenye Tume ya Katiba,”alisema.
Bukoba
Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Saidia Wazee Karagwe (Sawaka) Clement Nsherenguzi, alisema: “Ni muhimu kuonyesha kuwa tumeungana kweli kwa kuwa na taifa moja la Watanzania na kuondoa ubaguzi unaojionyesha katika masuala mbalimbali ikiwamo matukio yanayohusisha viongozi wa kitaifa.”
Naye Katibu wa Chama cha Walemavu, Manispaa ya Bukoba, Sweetbert Mshanga alisema: “Muungano kati ya nchi hizo umesaidia kujenga amani na mshikamano pamoja na kuwa ni wananchi wanaofahamu matunda ya moja kwa moja yanayotokana na Muungano huo.”
Alibainisha kuwa faida za kuungana ni kubwa ikilinganishwa na hasara ambayo ingepatikana kwa kutoungana, huku akitaka wananchi waelezwe wazi faida na matunda ya Muungano.
Akitoa maoni yake kuhusu miaka hamsini ya Muungano, Mwenyekiti wa Serikali ya Kitongoji cha Kajure katika Kisiwa cha Bumbire, wilayani Muleba, Deogratias Mutebwa alisema kuwa ni makosa kutaka kuua Muungano kwa visingizio vya kero zilizopo alizosema zinaweza kufanyiwa kazi bila kuvunja Muungano na kuwa muundo unaofaa ni serikali mbili.
Mara
Damiani Thobias ambaye ni Mkurugenzi wa shirika lisilo la kiserikali la Sederec, wilayani Serengeti alisema kwamba Muungano haufai kuendelea kukumbatiwa kwa kuwa hauna tija kwa wananchi.
“Kuna upungufu katika muundo wa serikali mbili, ndiyo maana wananchi wakatoa maoni ya muundo wa serikali tatu unaolenga kutatua kero hizo, kama unajengwa na nchi mbili, iweje nchi moja isionekane?”alihoji.
Nashoni Mkondya Mwenyekiti wa Mtaa wa Bomani mjini Mugumu (CUF)alisema: “Wajumbe wa Bunge la Katiba wanahoji uhalali wa maoni ya waliotaka serikali tatu, mbona hawahoji uhalali wa Rais Kikwete aliyechaguliwa na watu wachache kuwa Rais kati ya Watanzania waliopo na wao mbona ni wachache kuliko walioko nje lakini wanajiona halali.
Aidha, aliomba wajumbe watambue kuwa kujadili sera ya chama ya serikali mbili wakaacha maoni ya wananchi ni kutokujua nini wanafanya kwa kuwa Katiba ni juu ya vyama na ndiyo inaweka vyama lakini sera ya vyama haviweki katiba.
Iringa
 Mhadhiri Msaidizi wa Chuo Kikuu cha Ruaha (RUCO), mkoani Iringa, Gotrib Mgaya, alieleza kushangazwa na mjadala wa Bunge la Katiba unaoendelea kwa sasa na kusema wanaopendekeza serikali mbili wanapaswa kuja na hoja ya kuitaka Zanzibar ibadilishe Katiba yake ya mwaka 2010. 
“Kwa maoni yangu Rasimu ya Pili ya Katiba iliyotolewa na Tume ya Jaji Joseph Warioba imebeba maoni ya wananchi na ushahidi upo wa kutosha licha ya wabunge kuupinga. Mimi nadhani muundo huo unatibu matatizo ya muda mrefu ya Muungano,” alisema Mgaya na kuongeza:
“Muundo huu ulizingatia mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar ya 2010 ambayo imetamka kuwa Zanzibar ni nchi na kumpa mamlaka Rais wake kuwa na uwezo wa kuunda vikosi vya ulinzi, hatua hiyo imepunguza nguvu kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.”
Pwani
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mariam Halfani, Bosco Mfundo, Amina Hussein, Mwantumu Shaaban, Jesca Laizer, George Bundi na Machapula Donard walisema katika miaka 50 ya Muungano udhaifu uliojitokeza ufanyiwe kazi.
Walisema endapo pande zote zitaridhiana na kukubali kufanyika marekebisho itawezesha kupata suluhisho la kudumu na kuondoa manung’uniko ya wananchi wa nchi washirika za Tanganyika na Zanzibar.
Naye George Bundi alisema: “Mimi nafurahi miaka 50 sote tunasherehekea Muungano, lakini zipo changamoto kila siku zinaelezwa kuhusu huu Muungano, sasa basi wakati huu zifanyiwe marekebisho ili upande mmoja usiwe na manung’uniko. Sasa kwa nini wanakataa wazi Tanganyika siyo nchi? Wakisema hivyo basi hata huo Muungano uliopo ambao ni wa pande mbili za nchi ya Tanganyika na Zanzibar nao haupo.”
Imeandikwa na Haika Kimaro, Geofrey Nyang’oro Phinias Bashaya,  Anthony Mayunga,  Joyce Joliga, Songea Josephine Sanga, Julieth Ngarabali-MWANANCHI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post