KUHUSU MAUAJI YA WATU WATANO KWENYE MAPIGANO YA WAFUGAJI NA WAKULIMA WA SHINYANGA NA TABORA

Wakuu wa mikoa ya Tabora na Shinyanga kulia ni Bi Fatma Mwasa, kushoto ni Ally Nassoro Rufunga wakielekea eneo la tukio katika kijiji cha Isakamaliwa wilaya ya Igunga mkoani Tabora wakati kamati za ulinzi na usalama za Tabora na Shinyanga zilipokutana wilayani Igunga katika kijiji cha Magogo na Isakamaliwa.

Siku chache tu baada ya kutokea mauaji ya watu watano katika eneo la mpaka wa mkoa wa Shinyanga na Tabora kufuatia mapigano kati ya wakulima na wafugaji kutoka wilaya ya Kishapu na Igunga,wakuu wa mikoa hiyo wameunda tume ya watu 18 ili kuchunguza chanzo cha mgogoro wa kugombea ardhi kati ya wakulima na wafugaji ambao umesabisha viofo na uharibifu wa makazi na  watu.

Kufuatia mauaji hayo kamati za ulinzi na usalama za mikoa ya Shinyanga na Tabora  zikiongozwa na wakuu wa mikoa hiyo,jana zilikaa katika kijiji cha Magogo ambako vurugu hizo zimetokea na kuazimia kuundwa kwa tume ya watu 18 ili kuchunguza chanzo cha mgogoro huo.

Wakitoa taarifa baada ya  kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Ally Nassoro Rufunga na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Bi Fatuma Mwasa walisema serikali imelaani vikali vitendo hivyo vilivyofanywa na wafugaji wa jamii ya Kitaturu na kusema ni vitendo visivyovumilika kwani siyo desturi ya Watanzania na kwamba serikali imetoa salamu za pole kwa wafiwa na itahakikisha majeruhi mmoja anahudumiwa.


Wakuu hao wa mikoa walisema pamoja na kuundwa tume ya kuchunguza chanzo cha mgogoro huo pia kikao hicho kimeazimia kuwa wafugaji walioko katika kijiji cha Magalata wilayani Kishapu mkoa wa Shinyanga wabaki kwenye eneo lao na wasivuke mto Manonga kulisha ng'ombe wao na kwamba
wakulima walioko katika vijiji vya Magogo na Isakamaliwa wilaya ya Igunga mkoani Tabora wabaki huko na wasivuke mto Manonga.

Aidha walisema kwa upande wa wakulima walioharibiwa makazi yao waendelee na shughuli zao kama kawaida katika vijiji vya Magogo na Isakamaliwa mkoani Tabora na kuongeza kuwa ulinzi wa wananchi wa vijiji vya Magogo na Isakamaliwa umeimarishwa kwa kuongeza askari polisi ili kuhakikisha usalama wa eneo hilo unakuwepo.

Kikao pia kimeazimia waharibifu wa makazi ya watu na  wauaji wakamatwe ndani ya siku saba na kwamba halmashauri zote mbili za Igunga na Kishapu zihakikishe zinaboresha sheria ndogo ili kuwaadhibu wanaokiuka utaratibu wa mipaka.

Katika hali ya kusikitisha Jumamosi wiki iliyopita kulitokea mapigano ya wakulima na wafugaji  katika kijiji cha Isakamaliwa kilichopo mpakani mwa wilaya ya Kishapu mkoa wa Shinyanga na wilaya ya Igunga mkoa wa Tabora na kusababisha watu watano kupoteza maisha baada ya kuchomwa mikuki  wakati wakigombea  mipaka ya malisho na eneo kwa ajili ya kilimo.

Wakizungumza na waandishi wa habari baadhi ya wafugaji  walisema mapigano hayo  yametokana na wakulima kulima mazao  maeneo yote na kusababisha wao  kukosa maeneo ya malisho na kwamba, pindi wanap kwenda kuchunga mifugo  hunyang’anywa na wakulima huku wafugaji nao wakieleza kuwa siku hiyo baada ya ng’ombe zaidi ya 3000  kuswagwa na wakulima  na kupelekwa wilaya ya Igunga kwa madai kuwa mifugo inaingia kwenye mashamba yao na kula mazao,kitendo hicho kiliwakera  wafugaji  na  ndipo  mapigano hayo yaliibuka na kusababisha vifo vya watu watano sambamba na kuharibiwa kwa makazi ya watu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post