RASI AUA MTOTO KWA KUMPIGA NYUNDO KICHWANI HUKO TARIME

Mchinja nguruwe  katika Kitongoji cha Sokoni Mji mdogo wa Sirari, Tarime Ezekiel Magige  (39) amelazwa katika Hospitali ya Wilaya ya Tarime baada ya kupigwa mawe na wananchi wenye hasira kali.

Alishambuliwa hivyo  baada ya kumuua mtoto wake, Julias Ezekiel (2)  kwa kumpiga nyundo kichwani.

Magige ambaye anajulikana pia kama Rasi, kwa sasa ana majeraha mengi mwilini anayotibiwa hospitalini hapo.
Kamanda wa Polisi Tarime /Rorya,  Justus Kamugisha alithibitisha kutokea kwa tukio hilo.

Alisema Magige  kwa sasa yupo chini ya ulinzi wa Polisi hospitalini hapo, akipatiwa matibabu. Alikiri mtu huyo  kupigwa na wananchi baada ya kumuua mwanawe huyo.

"Magige yuko chini ya ulinzi wa Polisi hospitalini baada ya kushambuliwa na wananchi wenye hasira baada ya kumuua mwanawe kwa kumpiga na nyundo kichwani na usoni, tukio hili lilitokea Februari 28 mwaka huu jioni katika Kitongoji cha Sokoni  huko Sirari," alisema Kamanda Kamugisha.

Alisema uchunguzi wa tukio hilo, unaendelea ili kubaini chanzo cha mauaji hayo. Alisema mtuhumiwa huyo atafikishwa mahakamani, kujibu mashitaka ya mauaji hali yake itakapokuwa nzuri, kwani kwa sasa ni mbaya na hajitambui.

Wakazi wa Kitongoji cha Sokoni, Sirari, waliohojiwa kwa nyakati tofauti, walidai mtuhumiwa huyo  alikuwa mfuga nguruwe na mchinjaji na pia alikuwa akijishughulisha na kubeba mizigo katika Kituo cha Forodha  cha Mamlaka ya Mapato (TRA) cha Sirari.

Pia, walidai kuwa kulikuwa na migogoro ya kati ya mtu huyo na mke wake. Hata hivyo,  hawakufafanua ni aina gani ya migogoro hiyo.
Credit-Eddy blog

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post