MAISHA PLUS KUANZA LEO USIKU TBC1Vipindi vya televisheni vya shindano la Maisha  Plus kuanza kuonyeshwa leo usiku  katika kituo cha televisheni, TBC1. Akizungumza na wanahabari jijini Dar, Mratibu wa Mashindano hayo, Masoud Ali ‘Kipanya’ alisema vipindi hivyo vitaonyesha hatua za awali ambazo ni usaili na mpaka kupatikana kwa washiriki 30 waliobahatika kuingia kijijini.

“Tutaanza kuwaonyesha kipindi chetu kuanzia leo hii saa nne na dakika tano usiku, kipindi kitaanza kwa kuonyesha hatua za mwanzo kabisa za mashindano haya,” alisema Kipanya. Alifafanua akisema kuwa vipindi 10 vya mwanzo vitaonyesha mchakato mzima wa upatikanaji wa vijana 18 kutoka Tanzania watakao ungana na vijana wengine 12 kutoka Uganda, Kenya, Rwanda na Burundi zitakazotoa washiriki watatu kwa kila nchi.

Usaili wa mwaka huu ulikuwa tofauti na miaka mingine ambapo orodha ya washiriki 40 ilitengenezwa na ikagawanywa katika makundi mawili ambapo kundi la kwanza lilikwenda mkoani iringa kuishi kwenye vijiji vya huko na kushiriki shughuli za kijamii. Kundi la Pili litaenda visiwani Zanzibar ambalo pia litashiriki utamaduni wa kila siku wa kimaisha wa visiwani humo ambapo ni washiriki tisa tu katika kila kundi watachukuliwa na watachujwa kutokana na jinsi walivyoyamudu maisha ya huko.

“Vijana wakiwa huko katika vijiji vya kweli watakuwa wakishiriki shughuli za kilimo, usafi, za kiafya na nyinginezo kabla hawajaingia katika kijiji cha Maisha Plus”, alifafanua Kipanya. Baada ya kundi la kwanza na la pili kutoa washiriki tisa kila kundi, washiriki 18 watakuwa wameshapatikana, na sasa nchi za zikishapata washiriki wake 12, idadi ya washiriki 30 itaingia kijijini cha Maisha Plus katikati ya mwezi huu.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post