Mwanafunzi
wa darasa la kwanza Shule ya Msingi Jangwani, Manispaa ya Sumbawanga
amechomwa moto mikono yake miwili, kutokana na tuhuma za kudokoa njegere
zilizokuwa zikichemka jikoni.
Kamanda
wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Jacob Mwaruanda amethibitisha mkasa huo
aliouita ni wa kikatili huku akimtaja mtuhumiwa kuwa ni Anifa Lunyerere
(18), mkazi wa Kitongoji cha Bangwe, Manispaa ya Sumbawanga.
Kamanda
Mwaruanda alisema Lunyerere alimchoma mikono mtoto huyo (jina
limehifadhiwa) wiki iliyopita katika kitongoji hicho cha Bangwe saa sita
mchana.
Kwa
mujibu wa Kamanda Mwaruanda, mtoto huyo alipohojiwa alidai alifikia
uamuzi huo wa kudokoa njegere baada ya kuzidiwa na njaa, kwani alikuwa
ametoka shuleni ambako alikuwa hajala chochote.
“Mtoto
huyu alieleza kuwa wifi yake huyo amekuwa na tabia ya kumfanyia vitendo
vya kikatili mara kwa mara kama vile kumng’ata mgongoni hata kama
hajakosea kitu chochote,” alidai Kamanda Mwaruanda.
Mtuhumiwa
huyo anashikiliwa Polisi kwa mahojiano na anatarajiwa kufikishwa
mahakamani wakati wowote baada ya uchunguzi wa awali wa shauri lake
kukamilika.
Chanzo;Habari Leo