KUTANA NA RAIS HUYU ANAYENYOA VIDUKU,WANANCHI WAPATA WAKATI MGUMU

Wanaume Korea Kaskazini wanakabiliwa na mtihani mpya katika taifa lao; wa kunyoa nywele kwa mtindo ulioamuliwa na rais wao.
Watake, wasitake kuanzia sasa kila mwanamume atalazimika kunyoa nywele zake kwa mtindo anaoupenda Rais Kim Jong- un.
Kiongozi huyo kijana, aliyerithi wadhifa huo baada ya kifo cha baba yake, hana mzaha hasa kutokana na nia yake ya kujenga mfumo mpya wa utawala ambao matakwa yake tu ndiyo ya kufuatwa.
Ni wiki mbili sasa tangu serikali ya nchi hiyo kutoa agizo linalowataka wanaume kunyoa kama rais wao, huku wanawake nao wakielekezwa kutengeneza nywele zao kwa aina 18 tofauti na si zaidi ya hapo.
Hilo ni moja ya maagizo yenye utata kuwahi kutolewa chini ya utawala wake, ambapo amekuwa akifanya jitihada za kujijengea mizizi, ikiwamo kuwaondoa na kuwaadhibu wale waliokuwa katika utawala wa baba yake wanaoonekana kutokubaliana na aina yake ya uongozi.
Mapokezi tofauti
Hata hivyo, japokuwa staili yake ya unyoaji wa nywele imekuwa sehemu ya utambulisho wake na inafahamika na kila mmoja, agizo hilo limekuwa na mapokeo tofauti.
“Namna ya unyoaji wake wa nywele inavutia, kwa wanaoipenda. Lakini haiwezi kumpendeza kila mmoja atakayeiiga kwa kuwa maumbo ya vichwa yako tofauti kutokana na maumbile,” alieleza raia mmoja akinukuliwa na Radio Free Asia ya Korea Kusini.
Raia mwingine wa Korea Kaskazini ambaye anaishi nchini China, alieleza kwamba aina hiyo ya unyoaji nywele kwa raia waliopo China inaweza kuonekana kama uhuni.
“Hadi katikati ya miaka ya 2000 tulikuwa tukiitaja aina hiyo ya unyoaji wa nywele kama ‘mtindo wa wahuni wa China,” alisema raia huyu alipohojiwa na gazeti la Korea Times.
Hadi sasa, wanaume wa Korea Kaskazini wana aina 10 za unyoaji zilizowahi kuamriwa na Serikali yao.
Wanaume wamekuwa wakitakiwa kuwa na nywele fupi za wastani zenye urefu wa inchi mbili na wametakiwa pia kuzipunguza kila baada ya siku 15.
Via>>Babamzazi.com

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post