HUU NDIYO UJUMBE WA BABA MTAKATIFU FRANCISCO KWA KIPINDI CHA KWARESMA 2014

Mama Kanisa anakianza kipindi cha Kwaresima, yaani siku arobaini za toba na wongofu wa ndani; kusali na kufunga; kusoma na kulitafakari Neno la Mungu pamoja na kumwilisha imani katika matendo, kwa Jumatano ya Majivu. Waamini wanakumbushwa kwamba, wao ni mavumbi na mavumbini watarudi tena.


Hizi ni nyakati za toba na zimewekwa na Mama Kanisa kwa ajili ya mazoezi ya maisha ya kiroho; zinajikita katika liturujia ya toba, kuhiji kama ishara ya toba, kujinyima kwa hiyari kama sehemu ya kufunga na kutoa sadaka kwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii; ni mwaliko wa kushiriki kidugu kazi za mapendo na kimissionari zinazotekelezwa na Mama Kanisa.

Ujumbe wa Kwaresima kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko kwa Mwaka 2014 unaongozwa na kauli mbiu “Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, Jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba, ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake”. Huu ni mwaliko kwa waamini kuonesha moyo wa ukarimu kwa jirani zao kama ilivyokuwa nyakati za Mtakatifu Paulo aliyewahimiza Wakorintho kuwasaidia ndugu zao waliokuwa wanateseka mjini Yerusalemu.

Baba Mtakatifu katika tafakari hii anaonesha jinsi ambavyo Mwenyezi Mungu ambaye ni tajiri na mwingi wa rehema kwa njia ya Yesu Kristo, Mwanaye wa pekee amejinyenyekesha na kuwa maskini, ili aweze kuwa karibu na binadamu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho. Hiki ni kielelezo cha upendo wa Mungu ambao ni neema na baraka inayotolewa kwa binadamu anayependwa na Mwenyezi Mungu, kiasi cha hata Kristo kujisadaka maisha yake.

Huu ndio upendo unaoshirikisha, unajenga na kuimarisha umoja na udugu kwa kuvunjilia mbali kuta za utengano. Kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, Mwenyezi Mungu amefikiri na kutenda kama binadamu katika mambo yote isipokuwa hakutenda dhambi.

Kwa njia ya umaskini wa Yesu, Mwenyezi Mungu amependa mwanadamu aweze kutajirika, hii ndiyo mantiki ya Fumbo la Umwilisho na Fumbo la Msalaba. Alibatizwa mtoni Yordani si kwa vile alikuwa anahitaji toba, wongofu wa ndani na msamaha, bali alipenda kuonesha mshikamano wa dhati na binadamu mdhambi kwa kujitwika dhambi zake mabegani mwake, ili aweze kuwafariji, kuwaokoa na kuwakomboa kutoka katika lindi la dhambi na mauti.

Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake wa Kwaresima kwa Mwaka huu anasema, Yesu alijifanya kuwa jirani na Msamaria mwema, kwa kuguswa na mahangaiko ya binadamu, ili hatimaye, aweze kumwonjesha huruma na mapendo yanayobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Utajiri wa Yesu unajionesha kwa namna ya pekee kwa kumtegemea Baba yake wa mbinguni, katika kutekeleza mapenzi yake na hatimaye kuvikwa taji la utukufu. Yesu anatambua kwamba, ni Mwana pekee wa Mungu, Masiha anayewaalika wafuasi wake kujitajirisha kutoka kwake na kushiriki udugu na kujitahidi kuchuchumilia utakatifu wa maisha kwa kuishi kama watoto wa Mungu na ndugu zake Kristo.

Kila wakati Mwenyezi Mungu anaendelea kumkomboa mwanadamu kutoka katika umaskini wake kwa njia ya umaskini wa Yesu, kwa kuonja na kuguswa na umaskini wa jirani zao tayari kujifunga kibwebwe kusaidia kupambana na umaskini: wa hali, kipato na maadili. Umaskini ni kielelezo cha kukosa imani, mshikamano na matumaini. Umaskini wa kipato unawakumba wote wanaoishi katika mazingira ambayo ni kinyume kabisa cha utu na heshima ya binadamu.

Hawa ni watu wanaopokonywa haki na mahitaji msingi kama vile: chakula, maji, malazi, huduma bora za afya, fursa za kazi na ajira, maendeleo na ukuaji wa kitamaduni. Kanisa linaendelea kujisadaka kwa ajili ya kupambana na umaskini wa kipato katika mikakati yake ya kichungaji inayopania kumkomboa mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa linaiona na kuitambua sura ya Kristo miongoni mwa maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa Jamii. Kanisa linapania kuhakikisha kwamba, utu na heshima ya binadamu vinaendelea kupewa kipaumbele cha pekee kwa kukomesha ubaguzi ambao wakati mwingine ni chanzo kikuu cha umaskini. Kanisa linahimiza matumizi bora ya rasilimali ya dunia kwa ajili ya ustawi na maendeleo ya wengi. Jamii iongozwe katika misingi ya haki, usawa, kiasi na ushirikiano.

Baba Mtakatifu Francisko anasema kuna umaskini wa kimaadili, unaomfanya mwanadamu kuwa ni mtumwa wa dhambi, ulevi wa kupindukia, mcheza kamari na mtazamaji wa picha za ngono. Hili ni kundi la watu lililopoteza dira na mwelekeo wa maisha kwa kukata tamaa! Ni watu wanaoogelea katika utupu kwa kukosa fursa za ajira pamoja na kuendelea kudhalilishwa utu na hehima yao kama binadamu: wanakosa chakula na malazi; hawana haki ya kupata huduma bora katika sekta ya elimu, afya na maendeleo. Matokeo yake ni watu kuelemewa mno na umaskini wa kimaadili kiasi hata cha kutema zawadi ya maisha!

Umaskini huu ni chanzo kikuu cha myumbo wa uchumi kimataifa na matokeo yake ni umaskini na utupu wa maisha ya kiroho. Hali hii inajionesha pale mwanadamu anapomn’goa Mwenyezi Mungu katika maisha na vipaumbele vyake, kiasi hata cha kutema upendo na huruma yake. Hapa mwanadamu anadhani kwamba, anaweza kujitegemea mwenyewe na wala haitaji msaada kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Lakini ikumbukwe kwamba, ni Mungu peke yake anayeweza kukomboa na kumwokoa mwanadamu.

Baba Mtakatifu anasema, Injili ni dawa inayoponya umaskini wa maisha ya kiroho, changamoto na mwaliko kwa kila Mkristo kuhakikisha kwamba, anashiriki kutangaza Injili ya Kristo katika medani mbali mbali za maisha, ili watu waonjeshe upendo na huruma ya Mungu; ili hatimaye, waweze kushirikishwa maisha ya uzima wa milele. Waamini wawe ni watangazaji amini wa Injili ya Furaha inayojikita katika huruma na matumaini; mwanga na faraja kwa wote wanaotembea katika giza na uvuli wa mauti. Ni mwaliko wa kumfuasa Kristo aliyethubutu kuwaendea maskini; akaonesha sifa ya kuwa mchunga mwema kwa kumwendea Kondoo aliyekuwa amepotea, ili kumwonjesha upendo wake. Kwa kushikamana na Yesu, waamini wanaweza kuwa na ujasiri wa kushiriki katika mchakato wa Uinjilishaji Mpya na maendeleo endelevu.

Baba Mtakatifu Francisko katika Kipindi hiki cha Kwaresima anawataka waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuonesha ushuhuda wa pekee kwa maskini wa hali, maadili na maisha ya kiroho wanaokutana nao kila siku ya maisha yao, ili waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Yesu Kristo. Kwaresima ni muda muafaka wa kujisadaka kwa ajili ya kuwasaidia wengine, kwa kutambua kwamba, kwa njia hii pia tunafanya toba.

Waamini wanaweza kuwatajirisha jirani zao na hivyo kushiriki katika mchakato wa kuganga na kuponya umaskini unaomwandama binadamu. Ni matumaini ya Baba Mtakatifu Francisko kwamba, waamini wataweza kukitumia kipindi hiki cha Kwaresima ili kupata neema na baraka zinazobubujika kutoka kwa Kristo mwenyewe!

Ujumbe huu umehaririwa na
Padre Richard A. Mjigwa.
Idhaa ya Kiswahili ya Radio Vatican

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post