WIZI WA MABATI YA MBUNGE WAMTIA KICHEFUCHEFU MWENYEKITI WA CCM MSUKUMA,DIWANI ALIYEIBA AMEKIFEDHEHESHA CHAMA HUKO GEITA


Sakata la wizi wa mabati 14 ya jimbo yaliyotolewa na mbunge ,linalomkabili diwani wa kata ya Chigunga Hoja Mlyakado  limechukua sura mpya baada ya mwenyekiti wa chama hicho mkoani   Geita Joseph Msukuma kumtaka awajibishwe mara moja   kwa kitendo alichokifanya kwani ni fedheha mbele ya chama na mbele ya jamii nzima.
 

‘’Mimi kama mwenyekiti wa chama sijawahi kuona kiongozi ambaye ni mwakilishi wa wananchi na mwizi kama huyo inatakiwa awajibishwe mara moja na mimi nitahakikisha anawajibishwa kwa mujibu wa katiba ya chama cha mapinduzi”,alisema Msukuma.

“Kuanzia sasa hivi nitaagiza mamlaka zilizo chini yangu kuweza kulishughulikia suala hili kwa sababu nilikuwa silijui kama kuna kitu cha namna hii nashukru kunipa taarifa hizi ili hatua ziendelee kuchukuliwa”,aliongeza Msukuma.

Katika hatua nyingine  Mwenyekiti wa ccm mkoa wa Geita amesema chama cha mapinduzi hakikubaliani na viongozi wezi na wasiokuwa na maadili ndani ya chama na yeyote  akibainika  atachukuliwa hatua kali na ameahidi kuwagiza viongozi wa ngazi ya wilaya wachukue hatua kali dhidi ya diwani huyo mwizi haraka iwezekanavyo.

Ni hivi karibuni wakazi wa mji wa Geita na vitongoji vyake walishangazwa na kitendo cha Diwani wa kata ya Chigunga kuiba mabati 14 yaliyotolewa na mbunge wa jimbo hilo Mh Lolesia  Bukwimba na baadaye mbunge huyo kumwagiza diwani huyo ayarudishe  mabati hayo baada ya kukiri katika mkutano wa hadhara kuwa aliyachukua.

Wakiongea kwa nyakati tofauti na mwandishi wa habari hizi wananchi wa mkoa na vitongoji vyake wamesema kitendo cha diwani huyo kuiba mabati  14 na kufanya mkutano na kuwaambia wanananchi  kwamba ameleta mabati 86 na 14 yatakuja na mbunge si cha kiungwana na kitendo cha kuwafedhehesha wengine wanaoleta maendeleo  kwenye kata zao huku baadhi ya viongozi wakiwa wanaiba.

Kwa upande wa viongozi wa  vyama vya upinzani akiwemo kaimu katibu wa CHADEMA mkoani Geita Logers  Luhega amesema kitendo cha diwani huyo kuiba mabati kumi na nne na kumsingizia mbunge wake  si chakiungwana na kuwaomba viongozi wa CCM mkoa wa Geita kumchukuli hatua kali diwani huyo kwa wizi huo kwani amekidharirisha  chama na wananchi wamekosa imani naye.

‘’Kama diwani anafanya wizi kwa kuwaibia wananchi wake, je wengine wafanyeje? na kama hawatachukua hatua kali kwa diwani huyo tutahisi na wao wanahusika kuona mali za wananchi zinaibiwa”,alisema katibu huyo wa CHADEMA’.

Sakata la kuwepo kwa tuhuma za wizi wa mabati 14 zilianza kutolewa kwenye mkutano wa hadhara katika kijiji cha Kayenze baada ya wananchi kumhoji mbunge kuwa mabati 14 je amekujanayo? kama ambavyo diwani huyo aliwaahidi wananchi kuwa alileta mabati 86 na mengine mbunge atakuja nayo.

Kufuatia maswali ya wananchi,kitendo hicho kilimshitua mbunge huyo na kusema.....

 “Mimi nilitoa mabati 100 tena ya geji 28 nashangaa kuniambia nimekuja na mabati14 ndipo alipomsimamisha diwani huyo na kuanza kuzomewa na wananchi kwa kitendo alichokifanya cha kunisingizia kumbe yeye ameyachukua”,alisema mbunge huyo.


Na Valence Robert-Geita 

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post