Kamanda wa polisi mkoa wa SingidaGeofrey Kamwela |
Askari mmoja mhudumu wa wanyamapori mkoani Singida ameuawa na watu wengine 17 kujeruhiwa vibaya baada ya kuchomwa mishale, pinde na kukatwa mapanga na wananchi wenye hasira kali.
Askari huyo Athumani Jumanne (40) na watu wengine waliojeruhiwa wote wakazi wa Nduamughanga Wilaya ya Singida, wanadaiwa kuvamiwa na wananchi zaidi ya 300 kutoka kijiji jirani cha Handa-Chemba mkoani Dodoma wakitaka wapewe mifugo yao zaidi ya 150 iliyokamatwa kwenye hifadhi ya msitu.
Kamanda wa polisi wa mkoa wa Singida, Kamishina Msaidizi Mwandamizi Geofrey Kamwela amesema tukio hilo limetokea jana majira ya saa 7: 30 mchana, muda mfupi baada ya askari huyo na wenzake kukamata mifugo hiyo iliyokuwa inachunga kwenye hifadhi ya msitu wa asili wa Mgori.
Amesema wakiwa katika mapumziko, kundi la wananchi waliohamishwa kutoka kwenye hifadhi hiyo miezi miwili iliyopita, waliwavamia wakiwa na silaha mbalimbali za jadi na kuanza kuwashambulia.
Amesema askari huyo alikufa papo hapo, wakati wananchi 16 waliojeruhiwa wametibiwa Zahanati na kuruhusiwa, isipokuwa mmoja ambaye amelazwa katika hospitali ya mkoa kwa matibabu.
Kamanda Kamwela amesema mbali na kuua na kujeruhiwa, wananchi hao wamepora ng’ombe wengine 68, mbuzi 101, kondoo sita na punda watatu na kutoweka nao kama njia ya kulipiza kisasi.
Watu wawili wanashiliwa na jeshi la polisi na wengine wanaendelea kutafutwa kuhusiana na tukio hilo.
Credit-Chami wa matukio blog
Post a Comment