![]() |
Shimo lililochimbwa na wachimbaji haramu ndani ya Mgodi wa Almasi wa Mwadui, wachimbaji hao huchimba usiku wa manane kwa kutumia vifaa visivyo vya kitaalamu hivyo kuhatarisha maisha yao |
![]() |
Mkuu wa Mkoa akizungumza na wabeshi
hao(wachimbaji Haramu) alipowakuta eneo hilo hatari wakiendelea na shughuli
hiyo.picha zote na Magdalena Nkulu afisa habari ofisi ya mkuu wa mkoa wa Shinyanga
|
Kufuatia kukithiri kwa vitendo vya uchimbaji haramu wa madini katika mgodi wa almasi wa Mwadui,Mkuu wa mkoa wa
Shinyanga Ally Nassoro Rufunga amelaani na kukemea tabia ya baadhi ya wananchi
kuvamia maeneo ya migodi kwa lengo la kuiba mchanga wa madini kwa kuwa ni
kinyume cha sheria na kuahidi kuwasaidia wachimbaji hao haramu maarufu kwa jina
la Wabeshi katika kupata ajira mbadala.
Mkuu huyo wa mkoa ametoa
tamko hilo jana alipotembelea mgodi wa almasi Mwadui katika wilaya ya Kishapu na
kujionea hali ya uchimbaji haramu unavyofanyika katika mgodi huo pamoja na kuzungumza
na wachimbaji hao haramu.
Amesema kitendo hicho
ni hatari kwa maisha ya wananchi hao na kuongeza kuwa serikali mkoani Shinyanga
itawasaidia wachimbaji hao kutafuta shughuli mbadala ya kufanya na kuwataka
waachane na shughuli hiyo mara moja.
Rufunga amesema serikali
itahahakisha wanapata ajira halali kupitia viwanda vilivyopo na vinavyoendelea
kujengwa mkoani Shinyanga, kuwakopesha mitaji kwa mfuko wa maendeleo ya vijana
wa asilimia 5, pamoja na kufanya taratibu za kuwapatia maeneo madogo ili
wachimbe kihalali endapo wataachana na uchimbaji haramu wa madini.
Amesema aina hiyo ya uchimbaji
huo ni kuwaibia wawekezaji na kuwakwamisha kulipa mapato kwa serikali,kwani
nchi inapata kodi kutoka kwa wawekezaji waliopata leseni halali ya
uchimbaji,kodi ambayo inawanufaisha wananchi wenyewe katika shughuli za
maendeleo.
Naye Meneja Mkuu wa
Mgodi wa Mwadui Arlen Loehmer ameishukuru serikali kwa ushirikiano inaouonesha
kwa mgodi huo ikiwa ni pamoja na kusaidiana katika kujua na kutatua changamoto mbalimbali
na kwamba mahusiano hayo mazuri yanaimarisha
juhudi za uwekezaji.
Kwa upande wao wachimbaji
hao wamekiri mbele ya Mkuu wa Mkoa kuwa,ni kweli wanafahamu kazi hiyo siyo
halali na kuahidi kuachana nayo kama watasaidiwa shughuli mbadala kwani
wanafanya hivyo kujitafutia riziki kutokana na hali ngumu ya maisha na masharti
ya mikopo kuwa ni magumu.
Post a Comment