Ni hivi karibuni, Mji
wa Geita na maeneo jirani ulikubwa na taharuki ya aina yake,pale mtoto Shabani
Maulid (15) anaedaiwa kwamba alifariki dunia miaka miaka mitatu iliyopita,
alipoonekana akiwa hai katika Kijiji cha 14 Kambarage, Mtaa wa Mbugani.
Tukio hilo
lilizua hofu kwa wakazi wa Mji wa Geita huku waliowengi wakitaka kujua mtoto
huyo aliyekutwa amefariki dunia baada ya kupotea kwa siku nne mwaka 2011 na
mwili wake kuzikwa, inakuwaje leo hii anaonekana akiwa hai?
Tukio hilo
lililotokea Septemba mwaka huu linashuhudiwa na wazazi wa Shaban, ndugu zake,
jamaa na hata majirani wa eneo hilo ambao pia wanahoji, je aliyezikwa wakati
mwili wa mtoto huyo ulipookotwa ni nani na je mwili wake uko kaburini au la?
Maswali haya na
mengine, yalikosa majibu kwani baada ya kuonekana kwake, Shaban hakuweza
kuongea vizuri na alionekana kutofahamu kabisa Kiswahili, lugha ambayo kabla ya
kutoweka kwake aliifahamu vyema. Wakati huu mtoto huyu anaongea Kiha, japo nayo
kwa tabu.
Hali hiyo
iliwalazimisha wazazi wake kushirikiana na Jeshi la Polisi kumpeleka Haospitali
ya Wilaya ya Geita ili apatiwe matibabu, lakini ni kama hawakuona mtoto wao
akipata nafuu hivyo waliondoka naye na kuamua kumpeleka Kigoma Kambako
anapatiwa tiba za jadi.
“Niliamua nimpeleke
kwa waganga wa jadi huku nyumbani Kigoma na sasa hali inaendelea vizuri kwani
anaweza kuongea japo ni kwa muda mfupi kisha hunyamaza”, alisema baba mzazi wa
mtoto huyo, Maulidi.
Shaban alikuwa wapi?
Shaban hivi sasa
anaendelea vizuri na ‘tiba’ anayopata huko Kigoma na aliweza kuzungumza , huku akieleza kutoweka kwake, pia huko alikokuwa kwa
miaka mitatu, huku akiweka bayana kwamba hivi sasa anawatambua vizuri wazazi na
ndugu zake.
Alisema anakumbuka
Januari 1, 2011 aliondoka nyumbani kwao na kuelekea malishoni kuchunga mbuzi,
na wakati akiwa machungani ghafla lilitokea kundi la watu ambalo lilimzunguka.
Shabani anasema katika
kundi hilo alikuwamo mwanamke ambaye hakumtaja kwa maelezo kwamba anashindwa
kutamka jina lake, ambaye alimshika mkono na kumtaka waondoke eneo hilo.
“Walikuja watu wengi
wanaume kwa wanawake, ghaflla walinizunguka na nikasikia kama kizunguzungu na
akili yangu ikawa kama imezubaa,”alisema Shaban na kuongeza kuwa baada ya watu
hao kumzingira walimwamuru aswage mbuzi zake na kuwarudisha nyumbani.
“Niliongozana na watu hao tukiswaga mbuzi hadi
nyumbani, lakini wakati nafika hapo nyumbani hawakuweza kuniona japo mimi
nilikuwa naona kila jambo lilikuwa likiendelea,”anasimulia Shaban na kuongeza:
“Hao watu
walionizingira walijibadili sura na kuonekana kama majirani zetu na mimi pia
nilikuwa katikati ya kundi hilo ila wazazi hawakuweza kunitambua.
Alisema kuwa baada ya
kukabidhi mbuzi hao, watu hao waliondoka na yeye alibaki pale nyumbani akiwa na
mwanamke aliyemshika mkono, lakini wakati huo hakuwa akionekana wazi wala
kutambuliwa.
“Tulikaa pale nyumbani kwa nusu saa tangu
tulipofikisha mbuzi na baadaye tuliondoka na huyo mwanamke ambaye alikuwa
amenishika mkono, na tukarudi nilikokuwa nachungia na hapo tuliwakuta wale watu
wengine wakiwa wamesimama karibu na dimbwi la maji,”alisema Shaban.
Alisema baada ya
kufika katika dimbwi hilo walisimama katikati ya maji na baadaye alishtukia
akiwa chini ya bahari, ambako kulikuwa na senta (kituo) kubwa na watu wengi
wakiwa wanafanya shughuli mbalimbali.
“Tulisimama katikati ya dimbwi la maji, gafla
nilistukia niko katikati ya senta kubwa ambayo iko ndani ya maji kama
ziwa,”alisimulia mtoto huyo na kuongeza kuwa eneo hilo kubwa kama mji ama kijiji
ambako watu wanaishi. Hata hivyo kila alipotaka kutaja watu hao alishindwa
kutamka.
“Kuna watu wengi kwenye eneo hilo na mimi
nilistukia tu nikiwa huko na watu wenyewe sikuwajua kwani walikuwa wageni
kwangu,”alisema Shaban.
Hata hivyo alipohojiwa
wakati akiwa huko alikuwa akifanya nini, akila nini na watu wanaoishi huko
wanafanya shughuli gani, alishindwa kuongea na kumkabidhi baba yake simu.
Kwa upande wa baba
yake huyo anasema tangu alipompeleka mwanaye Shaban kwa mganga wa jadi
aliyemtaja kwa jina la Seleman Bundala, aliyeko Kijiji cha Nyankintonto, Kigoma
amekuwa akipata nafuu.
Alisema toka waanze
matibabu ya jadi kumekuwa na mabadiliko makubwa kwani,mtoto huyo alikuwa
haongei, lakini kwa sasa anaongea japo kwa shida na kwamba anaeleza alikokuwa
na jinsi alivyopelekwa.
“Hatoi maelezo mazuri kwani kuna wakati anaongea
vizuri na wakati anaonekana kama ulimi unakuwa mzito hasa tunapomuuliza maswali
kwamba ilikuwaje akatoka huko na alikuwa akifanya nini na watu waliomchukuwa ni
akina nani,”alisema Maulidi.
Alitowekaje?
Maulidi alitoweka
ghafla Januari 1, 2011. Wazazi wake wanasema siku hiyo aliondoka nyumbani
asubuhi na kupeleka mbuzi malishoni, na kwamba siku hiyo hakurudi, jambo
lililowatia mashaka wazazi wake hivyo kuamua kutoa taarifa polisi na kwa
uongozi wa kijiji.
Taarifa za kupotea
mtoto huyo zilienea kijijini hapo na ndipo walianza juhudi za kumtafuta na
baada ya siku nne, alikutwa amekufa ndani ya kisima cha maji.
“Mtoto wetu aliondoka
kwenda kulisha mbuzi siku ya sikukuu ya mwaka mpya muda wa saa nne asubuhi,
hadi inafika saa 12 jioni hakuonekana na badala yake tuliona mbuzi wakiletwa na
watoto wa majirani,”alisema Aziza Ramadhani mama mzazi wa Maulidi.
Aziza ndiye alikuwa wa
kwanza kumtambua mtoto wake katika Mtaa wa Mbugani eneo la Majarubani na wakati
huo alikuwa akitoka kwenye shughuli zake za kibiashara. Anasema alimwona Shaban
akikatiza barabara.
“Nilimuona mwanangu
akiwa anakatiza njiani ndipo nilimuita, Shabani mwanangu ni wewe? Niliposema
hivyo alishtuka, nikaamua kumsogelea huku nikimwita jina lake ndipo alipoitika
lakini hakunitizama usoni,” alisema mama huyo na kuongeza:
“Baada ya kuthibitisha
kwamba ndiye, watu walijaa na ndipo kwa kushirikiana na majirani tulitoa
taarifa polisi, na polisi wakaja kumchukua na kumpeleka hospitali huku akiwa
haongei na tulitumia ishara kuwasiliana naye”.
chanzo-Mwananchi
Post a Comment