WATU watatu wamefariki duniA baada ya dumu la petroli lililokuwa ndani ya nyumba walimokuwa kulipuka na kuteketeza nyumba katika
kijiji cha Nyangalata - Machimboni katika kata ya Lunguya wilayani Kahama
mkoani Shinyanga.
Kamanda wa polisi mkoa wa shinyanga ACP Evarist Mangalla amesema tukio hilo limetokea jana majira ya saa nne asubuhi na kuwataja waliopoteza maisha kuwa ni
Maria Peter (1), Hamis Masanja (1) na Saida Cosmas
(20).
Amesema vifo hivyo vilitokea wakati marehemu Saida Cosmas
alipokuwa akiwasha jiko kwa ajili ya kupika
chakula cha mchana ndipo aliingia shemeji yake aliyefahamika
kwa jina la Kulwa Bundala na kuanza kimimina Petroli kutoka
dumu moja kwenda jingine.
Kamanda Mangalla amefafanua kuwa mara baada ya Kulwa Bundala
kuanza kumimina petroli kwa kuhamishia ndani ya dumu jingine huku Saida
Cosmas akiendelea na pilikapilika za kuwasha moto ndipo moto mkubwa
ulitokea ghafla na kulipuka na kusababisha vifo vya watu watatu.
Hata hivyo baada ya kutokea kwa mlipuko wa moto Kulwa Bundala alifanikiwa
kutoroka na hivi sasa jeshi la
polisi linaendelea kumtafuta.