Mwanajeshi aliemuua Osama atoa neno......


Tangu kuuawa kwa kiongozi wa Kundi la Al-Qaeda Osama bin Laden kumekuwa na fununu nyingi zinazoeleeza mazingira ya kifo chake pamoja na ujumla wa maisha yake wakati akiwa mafichoni. Katika mfulilizo wa makala haya, Mwandishi George Njogopa amepitia simulizi za askari aliyemuua kiongozi huyo kama alivyozungumza na mwandishi mmoja wa habari nchini Marekani.

Akiwa mtu mwenye tabasamu na ucheshi wa mbali, askari (jina linahifadhiwa) anatoa maelekezo kwa mwandishi wa habari aliyetaka kujua historia ya maisha yake jeshini. Ndani ya mgahawa uliofurika watu waliochangamka kwa vinywaji, askari mwanamaji anaanza kueleza

namna alivyojiunga na Jeshi la Wanamaji la Marekani hadi kufikia nafasi ya kuwa mlenga shahaba mkuu.

Anasema anakumbuka kile kilichomsukuma kuchukua uamuzi wa kujiunga na jeshi ni kama sehemu ya hasira iliyomkumba baada ya kuachwa na mpenzi wake al iyedumu naye kwa kipindi kirefu.

“Unajua tukio la kuachwa na mpenzi wangu lilinivunja moyo sana… na ndiyo nikachukua uamuzi kwenda jeshini.

Anasema kuwa siku yake ya kwanza alipokwenda kuomba kazi anakumbuka alimwambia ofisa mmoja wa jeshi kuwa alikuja hapo kuomba kazi ya kulenga shahaba (sniper).

“Pale nilimkuta askari mfukuzi, mkufunzi akaniuliza unataka nini… nikamwambia nataka kuwa mlenga shahaha, lakini yeye akaniambia kuwa tayari walikuwa na walenga shabaha.

Hata hivyo alifaulu kuandikishwa na baadaye kupelekwa kwenye mafunzo yaliyimwongezea ujuzi wa kazi na hatimaye kuungana na vikosi vya wanajeshi wa maji vilivyosafiri sehemu mbalimbali duniani. Kama ilivyo kwa askari wengi wanamaji, askari huyu alishiriki kwenye operesheni mbalimbali za kijeshi ikiwemo zile zilizohusu katika nchi za Afghanistan na Iraq.

Anasema operesheni yake kubwa ya kijeshi ilikuwa nchini Afghanistan ambako vikosi vya Marekani vilivamia katika eneo hilo katika kile kilichoelezwa na kukabiliana na utawala wa Taliban ambao ulitajwa kuwa na ushirikiano wa karibu na Kundi la Kigaidi la Al-Qaeda.

“Uzoefu mkubwa wa kijeshi niliupata wakati nikiwa Afghanistan ambako nakumbuka nilishiriki kikamilifu kukabiliana na wanamgambo wa Taliban. Tulipofaulu kuwafurusha wanamgambo hao tuliendelea kubakia nchini huko kuimarisha hali ya usalama na kusaidiana na wananchi wa eneo lile kurejesha hali ya usalama.

“Kichwa changu kilikuwa tayari kimeshazoea mizinga na makombora, maana wakati mwingine umekaa sehemu ghafla unasikia kombora linavurumishwa mbele yako… Ghala nyuma unasikia mlio wa bunduki.. Kusema kweli nilijifunza mengi wakati nikiwa Afganistan.

Wakati huo Marekani ilianzisha operesheni za kukabiliana na Kundi la Al-Qaeda ambalo lililodaiwa kutekeleza tukio la kigaida katika majengo yake mjini New York na Washington.

Shabaha ya Marekani ilikuwa kukabiliana na kiongozi wa kundi hilo, Osama bin Laden ambaye wakati huo ilisemekana amejichimbia mafichoni katika Milima ya Afghanistan.

Marekani haikuishia kuingia kijeshi nchini Afghanistan pia iliivamia Iraq na hatimaye kuuangusha utawala wa Saadam Husen aliyekuwa akiongoza Chama cha Baath ambacho kilikuwa na uhusiano pia na baadhi ya makundi ya kigaidi.

Anakumbuka kuwa jinsi alivyorejea nyumbani Marekani na kisha kuungana na wanamaji wenzio ambao waliunda kikundi cha wataalamu wachache walikuwa na shabaha ya kuleta mageuzi ya utendaji ndani ya vikosi vya wanamaji hasa kwa kutumia uzoefu waliopata wakati wakiwa kwenye operesheni za kijeshi katika nchi za kigeni.

“Unajua ukishajiingiza kwenye mambo haya ya kulenga shabaha hujali tena lolote, wewe unachoona ni kwamba umeletwa duniani kwa kazi maalumu na hiyo kazi lazima uitekeleze kwa wakati uliopangwa,” anasema askari huyo akimwelezea mwandishi mmoja wa habari namna alivyoshiriki kwenye kikosi maalumu kilichoshiriki kwenye operesheni ya iliyofanikisha kuuawa kwa kiongozi wa Kundi la Al-Qaeda, Osama bin Laden.

Kwa masharti ya kutotajwa jina wala kuonyeshwa picha yake, askari huyo anasema kuwa, “Tulipomaliza kazi nchini Afghanistan tulirudi nyumbani na kuendelea na mazoezi yetu ya kuogelea

katika Ufukwe wa Miami. Tukiwa kule ghafla tukapata taarifa baadhi yetu tulihitajika kwenda Virginia kwa ajili ya kazi maalumu.

“Kusema kweli hatukujua nini tunachokwenda kukifanya maana tulielezwa kuwa kuna kazi ya dharura. Wengi wetu tukabaki tunahisi labda tunataka kupelekwa Libya, wengine wakasema labda tutaenda Japan kukabiliana na athari za kimazingira baada ya tetemeko kubwa la ardhi kulikumba taifa hilo.

Katika siku ya kwanza tulivyopata taarifa, kusema kweli walitudanganya. Tulizungushwa maeneo mbalimbali na kila mara maofisa wetu walikuwa wakitupa maelezo ya kutia matumaini wakisema kuwa tusiwe na wasiwasi tutaarifiwa punde kwani kulikuwa hakuna jambo lolote la kutisha.”

Anasema kuwa baada ya kukaa kwa siku kadhaa walipelekwa moja kwa moja hadi yaliko makao makuu ya upelelezi CIA, ambako walipokewa na maofisa wa ngazi juu aliyewagawanya kwenye vitengo bila kuwapa maelekezo yoyote.

“Wakati tunakwenda tuliambiwa tungekutana na Waziri wa Ulinzi, maofisa wa ngazi za juu wa jeshi pamoja na wataalamu wengine wa kijeshi. Tulipata hisia jambo tulioloitiwa huko huenda likawa kubwa. Tulipofika pale tulikusanywa kwenye chumba kimoja na baada ya muda alitokeza mwanamke mmoja ambaye kwa sura alionekana kuwa mtu jasiri na mwenye kuelewa kile anachokizungumza.

“Tuliona tumeletewa televisheni..vifaa vya kivita na pembeni kulikuwa na ramani kubwa ambayo hata hivyo ilifunikiwa na kitambaa . Hatukujua kile kilichokuwa kinaendelea. Yule mwanamke aliposimama ndipo pumzi ikatushuka,” Anaelezea kuwa walipatiwa maelekezo kuhusiana na sehemu ambayo inasadikika Kiongozi wa Al-Qaeda, Osama bin Laden ndiyo ilikuwa makazi yake.

“Yule askari wa kike akiwa katika hali ya kujiamini, alituonyesha ramani na kutufafanulia shabaha ya kuitwa kwenye chumba kile. Nilishtuka lakini kadiri nilivyomtazama yule askari niliamini kile alichokuwa akikisema. Tulionyeshwa nyumba moja ambayo iko pekee yake katika eneo la Abbottabad.

Baada ya hapo tukaingia kwenye mazoezi makali tukijifunza namna ya kuingia kwenye nyumba ile na namna tukavyoweza kumudu purukushani zozote zinazoweza kujitokeza.

Mafunzo yetu yalidumu kwa muda wa wiki kadhaa na kisha tulipangiwa siku ya kuondoka kuelekea Pakistan.

Anasema kuwa msafara wa kuelekea Pakistan alianzia nchini Ujerumani walikoweka kituo na kisha kuruka moja kwa moja hadi nchini Pakistan kupitia eneo la Jalalabad.

“Unajua wakati tunakatiza anga ya Pakistan niliingiwa na hofu sana pengine vikosi vya pale vingeilenga ndege zetu na kuzitungua maana kulikuwa hakuna taarifa zozote kwa Serikali ya Pakistan kuwa Majeshi ya Marekani yalikuwa yakiingia nchini humo.

Tulipita eneo lile na hatimaye kufika Abbottabad. Tulikuwa tumejipanga vya kutosha. Msafara wetu ulikuwa na helikopta, ndege za kivita pamoja na vifaru kukabili hali yoyote korofi ambayo ingejitokeza.

 

Nilishangaa kuona kile nilichoonyeshwa kwenye picha za satelaiti wakati nikiwa kwenye mazoezi Marekani ndicho nilichokishudia pale.

Tulishuka kwenye helikopta haraka na kisha kuizingira nyumba mara moja. Kuna wengine walitanda juu ya paa, wengine madirishani na wengi walikuwa angani kwenye helikopta.

Tulipofika mlangoni tulikuta tundu la risasi, tukashtuka kidogo, nikamwambia mwezangu acha woga hebu twende, nikasukuma mlango hadi ndani.

Wakati kabla hatujaingia ndani tulisikia sauti ikiita bla, blab la,,, kumbe ilikuwa sauti ya mmoja wa walinzi wa Osama ambaye alikuwa amevalia fulana nyeupe na pajama nyeupe pia.

Tulimdhibiti na kupanda hadi ghorofa ya pili ambako tuliwakuta kina mama wakiwa wanahangaika na kupiga kelele.

Hatukutaka kuwadhuru tuliwaweka chini ya ulinzi, nami nikaendelea kupanda juu hadi ghorofa ya tatu.

“Nilipofika chumba cha juu nilimwona mtu mmoja mrefu kupita wote, ndevu zake alikuwa ameonyoa kiasi. Alikuwa ameweka mikono yake begani kwa mwanamke mmoja ambaye baadaye nilikuja kugundua alikuwa mkewe Jamal.

Nadhani alikuwa anafanya vile kama njia mojawapo wa kujikinga. Alikuwa amevalia kofia na kuendelea kuzunguka huku na kule na yule mwanamke.

Nakumbuka alikuwa mwembamba. Pembeni yake kulikuwa na silaha aina ya AK 47, ambayo baadaye aliishika mkononi.

Binafsi sikutaka kupoteza muda, nilinyanyua bunduki yangu na kumiminia risasi mbili usoni na kisha nikamshudia namna alivyoanguka chini na kukata roho. Sikujali kama amekufa ala nilimmiminia risasi nyingine moja.

ALIYEKUWA kiongozi wa kundi la mtandao wa kigaidi la Al Qaeda, Osama bin Laden aliuawa Mei Mosi, 2011 na vikosi vya Marekani vilivyoyavamia maficho yake, Abbottabad, Pakistan. Tukio la kuuawa kwa kiongozi huyo lilipokewa kwa shangwe kubwa duniani kote ikiwamo Marekani kwenyewe.

Katika mfululizo wa simulizi hii askari aliyetekeleza mauaji hayo anaendelea kufahamisha jinsi alivyofanikisha operesheni hiyo.

Nyumba ya Osama bin Laden ilikuwa imezingirwa na askari wa Marekani waliofika kwenye eneo hilo nyakati za usiku wakiongozwa na rada maalumu iliyoratibiwa kutoka makao makuu ya jeshi, Pentagon. Wakati askari mlenga shabaha akiwa amepanda hadi ghorofa ya tatu, kulikuwa pia na askari wengine walioweka doria mlangoni.

Alipofika ghorofa ya tatu, askari huyo alimkuta Osama amesimama na mkewe huku wakiwa wamejihami kwa tukio lolote dhidi yao. Bila kupoteza muda askari huyo alimimina risasi mbili katika sehemu ya paji lake na ndipo Osama alipoanguka chini na kuaga dunia.

Aliongeza risasi nyingine katika sehemu ya mbavu zake na kisha akamsogelea mke wa Osama ambaye wakati huo alikuwa akilalama na kumtazama mumewe jinsi alivyokuwa akikata roho. “Niliongeza risasi ya tatu, kisha nikamfuata yule mama nikamkalisha kitandani…kumbe pembeni kulikuwa na mtoto mwenye umri kati ya miaka miwili ama mitatu. Huyu mtoto alikuwa wa Osama. Nilishtuka kidogo, nikamsogolea, maskini ya Mungu mtoto alilia kwa hofu na kutia huruma.
“Nilimchukua yule mtoto na kumweka kitandani kisha nikamnawisha maji na kuondoka kushuka chini kwa wenzangu”.

Anasema tukio hilo lilichukua sekunde 15.
Wakiwa bado wameshikwa na bumbuwazi baadhi ya askari walifika chumbani kwa Osama na kuukuta mwili wake ukiwa sakafuni. Pamoja na kwamba Osama alikuwa tayari amekwishafariki dunia, bado askari hao waliumiminia tena risasi mwili wa Osama na kisha baadaye waliushusha hadi chini na kuufunga katika mfuko maalumu.

Kisha waliendelea na kazi ya upekuzi ili kubaini kama kulikuwa na vitu vingine ambavyo Osama alikuwa akitumia kufanikisha maficho yake. Anasema kuwa walibaini vitu vingi zikiwamo kompyuta zilizowekwa katika kila chumba. Waliziharibu kompyuta hizo na kuchukua taarifa walizoona kwao ni muhimu.

“Lakini tulistaajabu kweli, maana kila chumba tulichoingia tulikuta kompyuta.”
Askari hao pia walibaini vifaa maalumu vilivyowekwa chini ya kitanda ambavyo hata hivyo taarifa zake hazikutolewa mara moja kama vifaa hivyo vilitumika kwa nini.

“Ndani ya nyumba ile kulikuwa na mambo mengi, maana pamoja na kushuhudia vifaa vya kunasia mawimbi ya sauti lakini kulikuwa na hifadhi kubwa ya chakula. Binafsi pia nilikuta lundo la dawa za kulevya aina ya Opium ambazo nadhani alikuwa akitumia Osama ama wafuasi wake maana tulizikuta katika vyumba vya chini.”

Baada ya operesheni ya kuikagua nyumba hiyo kukamilika, askari hao wakiwa na msafara wao walirejea hadi ilikokuwa kambi ya vikosi vya Marekani mjini Jalalabad kwa ajili ya kuwasilisha mwili wa Osama bin Laden pamoja na familia yake. Mkuu wa ngome ya Jalalabad alipewa taarifa ya operesheni hiyo na baadaye alifanya utambuzi kwa mwili wa Osama kabla ya kutoa taarifa yake ya mwisho makao makuu Washington.

Kamanda McRaven akiwa na ofisa wa CIA walichukua vipimo vya mwili wa Osama na kujiridhisha kuwa ndiye yeye aliyeuawa. Wakati wanachunguza waliona matundu mengi ya risasi katika sehemu za kifua hadi miguuni.

“Unajua nilipomuua tu, baadaye askari wengi walikuja. Kila mmoja alipiga risasi sehemu aliyojua yeye. Ndiyo maana utakuta mwili wake ulikuwa na sehemu nyingi ziizopigwa risasi.

Wakati mwili wa Osama ukisafirishwa hadi Jalalabad familia yake nayo ilikuwa kwenye msafara huo ambao bado ulifanywa kwa siri na uangalifu mkubwa kuhofia kuvuja kwa taarifa za kifo za kiongozi huyo kabla ya kutangazwa na Ikulu ya Washington.

“Wakati tukiwa Jalalabad nilimwona mke wa Osama, nikamfuata nikamuuliza je huyu ndiye aliyekuwa jamaa yako? Yule mama hakunijibu chochote. Aliendelea kububujikwa machozi. Nilichukua begi langu na kukuta kulikuwa na magazine ambayo ndani yake kulikuwa na risasi 27 ambazo zilikuwa hazijatumika.

“Nilimpa yule mama, nikamwambia nadhani ndani ya moyo wako kuna sehemu unaweza kuhifadhi kumbukumbu hii. Nilimwachia zile risasi na ndiyo ilikuwa siku yangu ya mwisho kuonana na mama yule, na zaidi ya yote sikujua kilichoendelea.”

Anasema kuwa aliendelea na shughuli zake za kawaida akisubiri amri ya kurejea nyumbani Marekani kwani kazi aliyotumwa nchini Pakistan alikuwa ameikamilisha. Anasema kuwa wakati akirejea toka Abbottabad njiani alitaniana na askari wengine waliokuwa wakiimba na kutoleana maneno ya kupongezana.

Binafsi hakutarajia kama taarifa za yeye kuwa ndiye aliyesitisha uhai wa Osama zingekuwa zimejulikana karibu kwa maofisa wote wa jeshi kwani hakujua kwamba kulikuwa na mawasiliano ya moja kwa moja yaliyokuwa yakifanyika wakati wa operesheni ya kumsaka kiongozi huyo.

“Tulipofika Jalalabad nilipokewa kwa furaha kubwa na kamanda McRaven ambaye alinikumbatia na kunipigapiga mgongoni kama vile mtoto aliyekuwa akipongezwa na mzazi wake baada ya kufanikisha jambo fuani. Pia wakati tukiwa kwenye ndege baadhi ya wahudumu walionyesha sura ya tabasamu kwangu na kuna wengine walinikumbatia na kunipongeza.

Taarifa za kuuawa kwa Osama ziliwasilishwa Ikulu ya Marekani ambayo hata hivyo tayari ilikuwa inajua kwani ilifuatilia moja kwa moja wakati wa operesheni hiyo iliyoendeshwa usiku wa kuamkia Mei Mosi, 2011.

Rais Barack Obama akiwa pamoja na maofisa wa usalama na mawaziri kadhaa walifuatilia operesheni hiyo toka chumba maalumu kilichonasa moja kwa moja matukio yote yaliyoendelea na baadaye kuthibitishwa kupitia fumbo la namba lilitolewa na maofisa wa usalama walioweka kambi katika mji wa Jalalabad.

“Sasa jambo la kustaajabisha kwangu ni kwamba siku ile niko sehemu nikifungua kinywa, mkononi nimeshika kikombe changu cha kahawa, na upande wa pili nimeshika sandwich nakula, ghalfa macho yangu yakaelekea kwenye runinga….. daah nikamwona Rais Obama anazungumza.

“Rais anautangazia umma kuhusu kuuawa kwa Osama… binafsi nikatupa macho pembeni naona mwili wa Osama, nikatua macho kwenye runinga namwona Rais akizunguzia kifo chake…. Kwa vile mie ndiye niliyemuua Osama, nikasema moyoni “najipongeza kwa kazi kubwa, tena ningali hai, ilikuwa kazi yenye weledi mkubwa na imefanywa kwa umakini mkubwa.”

“Ilikuwa faraja kubwa kwangu kuweza kuisaidia nchi yangu, watu wangu na wananchi wa New York ambao waliathiriwa vibaya na tukio la kigaidi la Septemba 11. Hii ni heshima kubwa maishani mwangu.

Sehemu ya mwisho ya simulizi hii itaendelea tena kesho ikimulika zaidi maisha binafsi ya askari huyo na kujua namna anavyoishi na familia yake.

Chanzo: Mwananchi Newspaper.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post