WANAFUNZI WOTE WALIOPATA DIVISION 0 (ZERO) KURUDIA MTIHANI MWAKA HUU...


           

Serikali imesema inaangalia utaratibu wa watahiniwa 240,903 wa kidato cha nne waliopata daraja sifuri katika matokeo yaliyotangazwa hivi karibuni, kurudia mtihani mwaka huu kwa gharama zake.

Aidha, imesema matokeo mabaya ya mwaka huu yamesababishwa na mambo makuu manane, kubwa likiwa ni wanafunzi waliopita bila kuchujwa katika mtihani wa kidato cha pili walioufanya miaka miwili iliyopita.

Naibu Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Philipo Mulugo alisema hayo jana alipozungumza na gazeti hili kuhusu hatua zitakazochukuliwa na Serikali kutokana na idadi kubwa (asilimia 60.6) ya watahiniwa wa kidato cha nne kufeli mtihani wa Taifa kwa daraja sifuri na hatima yao ya kujiuzulu.

Akifafanua, Mulugo alisema, “suala la kujiuzulu lipo nje ya mipaka yangu ya kazi kwa kuwa halihusishi wizara moja wala Serikali pekee. Lakini kuhusu hatua zitakazochukuliwa kwa waliopata sifuri, Serikali inafikiria warudie mtihani mwaka huu”.

Ingawa alisema wazo hilo halijapitishwa, lakini hivi sasa linajadiliwa kuona namna ya kuwasaidia watahiniwa zaidi ya 240,000 waliopata alama hiyo, kurudia mtihani wa Taifa kwa gharama za Serikali. Watahiniwa waliosajiliwa walikuwa 480,036.

“Katika kuchambua hilo, tumeangalia namna ya kuwalipia ada ya mtihani ambayo mwaka jana walilipa Sh 35,000 kila mwanafunzi, likipita hilo la kurudia mtihani, Serikali italipia ada hiyo na wataufanya kama watahiniwa binafsi,” alibainisha Mulugo.

Sababu za kufeli

Kuhusu matokeo mabaya, Mulugo alisema sababu kubwa ni kutokuwapo mchujo kwa watahiniwa waliopata chini ya asilimia 30 wakati walipofanya mtihani wa kidato cha pili na hali hiyo inaweza kujitokeza hata kwa watahiniwa wa kidato cha nne mwaka huu.

“Hawa ni waliofanya mtihani wakati mfumo wa kuwachuja walipokuwa kidato cha pili ulikuwa umeondolewa, walipita wote, iwe alipata F au A, na walipita kwa miaka miwili, hivyo hata mwaka huu athari zinaweza kutokea, ila watakaoingia kidato cha nne mwakani, walichujwa na sifuri zilikuwa zaidi ya 136,000, hivyo tofauti inaweza kuwapo,” alifafanua.

Hata hivyo, alisema matokeo hayo mabaya hayatarekebishwa kwa namna yoyote, ili kuongeza idadi ya watakaoingia kidato cha tano mwaka huu, bali watahiniwa 23,500 waliopata daraja la kwanza hadi la tatu ndio watakaoendelea.

Alisema watakaochukuliwa Ualimu ni wa daraja la nne ya alama 26 na 27 huku wenye alama 28 wakiachwa bila kuchukuliwa mwaka huu.

Kujiuzulu?

Akielezea shinikizo la kuwataka yeye, Waziri Dk Shukuru Kawambwa na Katibu Mkuu wa Baraza la Mitihani Tanzania (Necta), Dk Joyce Ndalichako wajiuzulu, Mulugo alisema suala hilo liko nje ya mipaka yake ya kazi kwa kuwa linahusisha Wizara zaidi ya moja.

“Si sahihi kulizungumza hilo la kujiuzulu, kwa kuwa liko nje ya mipaka yangu ya kazi, si suala la Wizara ya Elimu pekee, ni mtambuka na linashughulikiwa na wizara zaidi ya moja, hata hivyo hatua tayari zinachukuliwa kutafuta kwanza kiini cha tatizo na mpaka sasa tumegundua mambo manane.

Akiyataja, Mulugo alisema ni pamoja na jamii kutosaidia wanafunzi kufikia malengo, wanafunzi wenyewe, mitandao ya kijamii nje ya masuala ya elimu, wazazi, Sayansi na Teknolojia na Serikali katika mipango na sera, mwingiliano wa uwajibikaji kitaasisi (wizara zaidi ya moja, ikiwamo Tamisemi iliyo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu).

Kuhusu madai ya mtihani mgumu uliokuwa na mbinu za kitaalamu zaidi, Mulugo alisema hakuna mtihani mwepesi duniani na kuongeza, kwamba uwajibikaji wa wanafunzi katika elimu umefifia kutokana na uhuru mkubwa walionao kupitia mitandao ya jamii na vyombo vya habari, huku akidai baadhi wanaiga kwa kasi mabaya wanayoyaona humo na kuyahamishia katika mitihani.

Utungaji

Pia alieleza namna mtihani unavyotungwa na kubainisha, kuwa Necta huandika barua kwa Ofisa Elimu wa Mkoa akiomba walimu makini walio kazini, watunge maswali ya mwongozo wa mtihani na maswali hayo hupelekwa katika Baraza na huko walimu baadhi kuyapitia tena.

“Baada ya hapo walimu angalau wawili au watatu kutoka kila mkoa huweka kambi ya siku si chini ya 10 kuhakiki na kupitia maswali hayo, kisha Necta huunda kamati ndogo inayapitia miongoni mwao maswali yanakuwa mtihani na si nje ya hapo. Utaona anayetunga mtihani ni mwalimu anayemfahamu mwanafunzi,” alisema Mulugo.

Katika kusahihisha, kwa mujibu wa Mulugo, walimu makini kutoka kila mkoa huchukuliwa kwa uwakilishi na kupangiwa vituo vya kusahihisha mtihani, na walimu wa somo moja hukaa kituo kimoja tofauti na wa somo lingine na mwalimu mmoja husahihisha swali moja na kumpa mwenzake.

“Haiwezekani kumpendelea mtu, unakuta mtihani wa hesabu uko Kilimanjaro, Kiingereza uko Dar es Salaam, labda wa Kiswahili unasahihishwa Mbeya, sasa walimu wote wanakujua ama wakupendelee au kukuonea?”

Alisema na kusisitiza kuwa matokeo ya mwaka huu yalitokana na udhibiti wa wizi wa mitihani uliofanywa na Serikali na utaendelea miaka yote.

Aliitaka jamii kushirikiana kuwawezesha wanafunzi kufikia malengo ya elimu kwa kudhibiti katika matumizi ya simu, mitandao ya jamii na wizi wa mitihani na kuongeza kuwa suala la elimu linapaswa kuwa la wote, huku Serikali ikiwa ni mtunga sera na msimamizi.

Yamekuwapo malalamiko mengi kutoka kwa wananchi wa kada mbalimbali kuhusu kufeli kwa kiasi kikubwa wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka jana.
      Source Habari leo

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments