Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania (MAT), Dk. Stephen Ulimboka atoa tamko baada ya kimya kirefu



Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari nchini, Dk.
Stephen Ulimboka, akisaini tamko lake kwa watanzania ambalo lilisomwa kwa niaba
yake na Wakili wake, Nyaronyo Kicheere, Dar es Salaam. Kulia ni Wakili na
Kamishna wa Viapo, Rugemeleza Nshala. Tamko hilo alisaini Oktoba 07, jijini Dar
es Salaam.Picha na Joseph Senga
--
HATIMAYE Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania (MAT), Dk.
Stephen Ulimboka, amefunguka na kudai maelezo yote aliyoyatoa na
kurekodiwa kabla na baada ya kufika hospitali ni ya kweli.





Alisema alitoa maelezo hayo, akiwa na kumbukumbu sahihi na kuwataka
Watanzania, kupuuza wale wote wanaotaka kupotosha ukweli juu ya tukio
hilo.





Akisoma tamko hilo, kwa niaba ya Dk. Ulimboka, Wakili wa kujitegemea
Nyaronyo Kicheere alisema, amepewa jukumu la kuwasilisha tamko hilo, kwa
Watanzania kwa kuwa, Dk. Ulimboka yuko nje ya nchi akiendelea na
matibabu yake aliyoanza mapema, baada ya kutekwa na kuteswa na watu
wasiojulikana.



Pamoja na mambo mengine, Dk. Ulimboka amedai yuko tayari kuhojiwa na
kutoa ushirikiano kwa vyombo huru na makini vya uchunguzi, ambavyo
vitaundwa ili kuweza kubaini ukweli.





Akisisitiza uthibitisho wa madai hayo, Dk. Ulimboka alisema, maelezo
aliyoyatoa ambayo yamerekodiwa kwenye mtandao wa You Tube, ni ya kweli
na wakati anatoa maelezo hayo, alikuwa na kumbukumbu nzuri bila athari
yoyote pamoja na maumivu makali.





“Uthibitisho wa kumbukumbu nzuri, niliyokuwa nayo ni pale
nilipokutana na Juma Mganza, katika msitu wa Mabwepande asubuhi ya siku
ya tukio, pamoja na maumivu makali niliyokuwa nayo kila sehemu ya mwili
wangu, niliweza kumshawishi Mganza anifungue kamba za mikono nilizokuwa
nimefungwa…pia kukumbuka namba ya simu ya rafiki yangu Dk.Deogratius,
ambapo Mgaza aliweza kuwasiliana naye kumpa taarifa ya tukio hilo na
mimi kufikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili.





“Najua wapo watu ambao wamekuwa wakihaha kupindisha ukweli, lakini
wanasahau kuwa, niliweza kumshawishi Mganza hadi akashawishika
kunikaribia na kunisikiliza pamoja na hofu aliyokuwa nayo ya kukutana na
mtu aliyekuwa katika hali kama yangu.





Niliweza kukumbuka namba ya rafiki yangu, mambo hayo yanatosha
kuthibitisha nilichokisema ni ukweli na kuwa, utimamu na kumbukumbu
zangu ni sahihi,” alisema Dk. Ulimboka katika tamko hilo.



Akizungumzia tukio la kutekwa na kuteswa kwake kabla halijatokea,
alisema alikuwa na kikao na afisa wa Ikulu, Ramadhani Abeid Ighondu.





“Nathibitisha kuwa, Ighondu alitambulishwa kwetu kwa jina la Abeid na
kigogo mmoja, binafsi ninamfahamu sana huyu kwa sababu alikuwa akitumwa
mara kwa mara kuja kukutana na mimi na tumekutana mara kadhaa kabla ya
tukio lile.





“Tulitambulishwa kwake mimi na madaktari wenzangu, kuwa yeye ndiye
atakayehusika kuchukua madai na hoja za madaktari katika mgogoro wetu na
Serikali, nathibitisha kuwa, mfanyakazi huyu wa Ikulu, ndiye
aliyenipigia simu ambapo alikuwa akitumia namba (tunayo) na kuniita
kwenye kikao ambapo muda mfupi baadaye nilitekwa.





“Hakuna shaka, namtambua Abeid kwa sura na naamini kwa dhati kuwa,
afisa huyu bado yuko hai… mimi na wenzangu tuko tayari kutoa ushirikiano
kwa chombo huru kuhakikisha haki inatendeka.



“Naendelea kuthibitisha kuwa, Abeid ninamfahamu na hata akikamatwa
leo hii nitakwenda kufanya utambuzi, ninasikitika hatujasikia popote
kuwa, Abeid pamoja na washirika wake wamehojiwa pamoja na jamaa
waliotajwa mpaka sasa.



“Ninafahamu kuwa, ibara ya 14 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania, inatoa kinga kwa uhai wa kila mtu anayeishi katika nchi yetu,
tena inaitaka jamii kulinda uhai wa kila mtu, mimi Ulimboka Stephen,
ninafahamu kwamba nina haki ya kuishi na kuwa Serikali yangu na wananchi
wenzangu, wanajukumu la kuulinda uhai wangu.





Akijibu maswali ya waandishi wa habari kuhusu kwa nini Dk. Ulimboka
amemchagua yeye kuwasilisha tamko hilo, Wakili Kicheere alisema, imani
yake kwake ndiyo iliyopelekea yeye kupewa madaraka hayo.



Wakili Nyaronyo alitoa tamko hilo, kwa usimamizi wa mwanasheria
Rugemeleza Nshala, Oktoba 14, mwaka huu ili aliwasilishe kwa Watanzania,
lakini siku zote hizo alikosa ukumbi hadi jana alipopata nafasi katika
ofisi za Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRD).



Dk. Ulimboka alitekwa usiku wa Julai 26, mwaka huu na watu
wasiojulikana, ambapo aliteswa na kunyofolewa kuacha na kung’olewa meno
na baada ya hapo alisafirishwa kwenda nchini Afrika Kusini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post