Uchunguzi mauaji ya Kamanda Barlow utata mtupu

 Send to a friend

Frederick Katulanda, Mwanza
MKURUGENZI wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai nchini (DCI), Robert Manumba, amesema uchunguzi dhidi ya kifo cha aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Leberatus Barlow, bado ni mgumu, hivyo hana taarifa ya kuridhisha ili kutoa kwa vyombo vya habari.

“Jamani uchunguzi huu ni mgumu sana, bado tunahangaika hapa siwezi kusema lolote kwa sasa kuridhisha vyombo vya habari,” alieleza Manumba.

Manumba aliendelea,"Uchunguzi huo ni mgumu sana na hata watuhumiwa tunaowashikilia bado hawajaweza kutoa mwanga wa tukio hilo."

Liberatus Barlow aliuawa Oktoba 13 mwaka huu, saa 8 usiku kwa kupigwa risasi na watu wasiojulikana katika eneo la Minazi mitatu huko Kitangiri wakati alipopita kumsindikiza Mwalimu Dorothy Moses nyumbani kwake kutoka katika kikao cha harusi kilichofanyika Mtaa wa Rufiji.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, DCI Manumba alisema kamba kwa sasa bado wanahangaika na uchunguzi wa mauaji hayo na kwa hatua waliopo hana taarifa ya kuridhisha kutoa kwa vyombo vya habari.

Ni kutokana na ugumu wa uchunguzi kwa sasa jeshi lake halina taarifa rasmi kwa ajili ya kueleza juu ya uchunguzi huo jambo ambalo limeelezwa na wafuatiliaji wa masuala haya ya uchunguzi kama unatokana na mauaji hayo kupangwa vilivyo na watekelezaji wake.

"Polisi bado wanayo kazi ngumu katika uchunguzi huu na wala wasifikirie uchunguzi umekamilika kwa madai mauaji haya ni mapenzi, uchunguzi ni kazi ngumu, na unaweza kupata sababu ya kwanza ukadhani umemaliza kumbe muuaji alikutegesha ili unase hapo na yeye akizidi kujichimbia," alieleza mmoja wa ofisa wa Jeshi la Wananchi Tanzania (JWT) ambaye amekuwa akihusika na masuala ya uchunguzi.

Alisema mauaji haya yanaweza kuwa yamepangwa na askari wenyewe na kwa vile walitambua kuwa na mahusiano na mwanamke yule waliyemwita dada yake wakayaunganisha huko ili kujifisha na nia yao ovu, hivyo polisi na wote wanaofanya uchunguzi wanapaswa kuwa makini sana na uchambuaji wa taarifa za uchunguzi ili waweze kufanikiwa katika utafutaji wa wahusika.

"Uchunguzi wa polisi unaweza kuwa mgumu sana iwapo mauaji hayo yamepangwa na miongoni mwao na wao ndiyo wanaohusika na uchunguzi, ni lazima utawasumbua sana, sasa wanapaswa kuwa makini sana kwa kila hatua vinginevyo muda utaisha na hawataambulia kumnasa muuaji wa kweli," alizidi kufafanua ofisa huyo wa jeshi.

Wakati Manumba akieleza ugumu wa upelelezi ka sakata hilo, jijini Mwanza kumekuwa na uvumi unaoenea huku ukitaja baadhi ya majina ya watu wakihusishwa na tuhuma za mauaji hayo kwa madai kuwa wamekamatwa.

Watu ambao wamekuwa wakitajwa ni  aliyekuwa rafiki mkubwa wa mtuhumiwa aliyekamatwa. Anayedaiwa kukamatwa (jina linahifadhiwa) alikuwa diwani wa Chadema lakini  alisimamishwa uanachama kwa kupokonywa kadi kwa madai ya kukihujumu chama chake.

Wengine ambao wametajwa ni pamoja na mchezaji wa zamani wa timu ya Pamba na Yanga (jina linahifadhiwa) watu ambao DCI Manumba amekanusha kwamba hana taarifa za kukamatwa kwao.

Katika uchunguzi huo, polisi limeelezwa kushirikiana na vyombo vyote vya dola ambao ni Usalama wa Taifa, pamoja na Interpol kama alivyoeleza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Evalist Ndikilo kwamba vyombo vyote vya dola vipo katika uchunguzi wa kina wa suala hilo.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553
Previous Post Next Post