|
|
MWANAMKE mmoja aliyefahamika kwa jina la Subira Malefya (53),
mkazi wa kijiji cha Ipinda, kata ya Ipinda, wilayani Kyela, amelazwa
katika hospitali ya wilaya Kyela baada ya kuunguzwa vibaya mwili mzima
na mumewe usiku wa kuamukia juzi.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Katibu, tarafa ya Ntebela,
Cuthberty Mwalukama, akiwa amelala mwanamke huyo alimwagiwa mafuta ya
taa mwili mzima kabla ya kumwasha moto kwa kiberiti ikiwa ni usiku wa
saa 4:00.
Alisema baada ya mume huyo kufika nyumbani akiwa amelewa wakati huo
mkewe akiwa amelala na wajukuu zake, ndipo akaenda dukani kununua mafuta
ya taa kiasi cha lita moja na nusu na kiberiti, kisha kummwagia mkewe
na kumtia kiberiti.
Katibu tarafa huyo alifafanua kuwa mume wa mwanamke huyo ambaye ni
mwalimu mstaafu, Boniphace Mwakinyuke (64), yeye na mkewe walikuwa
pamoja klabuni siku hiyo, lakini mke aliwahi kuondoka, kitendo ambacho
kinadhaniwa kumkera mumewe.
Alisema baada ya tukio hilo, wananchi wa eneo hilo walitoa msaada wa
kumkimbiza hospitalini mwanamke huyo katika kituo cha afya Ipinda akiwa
mahututi na baada ya kupatiwa matibabu ya awali, walimkimbizia hospitali
ya wilaya kwa matibabu zaidi.
Aliongeza kuwa mbali ya wasamaria hao kumsaidia mwanamke huyo, pia
walimkamata mtuhumiwa huyo na kumfikisha katika kituo kidogo cha polisi
cha Ipinda kabla ya kupelekwa kituo kikuu cha polisi wilayani Kyela,
anakoshikiliwa kabla ya kufikishwa mahakamani kwa taratibu zaidi za
kisheria.
Naye mganga mkuu wa wilaya Kyela, Festo Ndungange, amekiri kumpokea
mgonjwa huyo ambaye amelazwa kwenye wodi namba 3 akisema wanajitahidi
kumhudumia kumpunguzia maumivu anayoyapata.
|
|
Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa
Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553