Wanaoichochea na kufadhili vurugu kukamatwa


Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi
Serikali imepiga marufuku mihadhara yote inayochochea vurugu za kidini na kutangaza kuwakamata wote wanaofadhili vikundi hivyo.

Tamko hilo limetolewa na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi  wakati akizungumza na waandishi wa habari jana, jijini Dar es Salaam.

Alikuwa akizungumzia matukio ya vurugu zilizofanywa na baadhi ya watu wanaoaminika kuwa Waislamu katika miji ya Zanzibar na Dar es Salaam, yaliyotokea  juzi.

Alisema mihadhara yote ya kidini imepigwa marufuku kwa muda wa mwezi mmoja huku serikali ikifanya  uchunguzi ili kubaini watu wanaofadhili vurugu hizo kutoka nje na ndani ya nchi.

Dk. Nchimbi alisema Serikali imejipanga kuhakikisha inatumia nguvu pamoja na vyombo vya sheria endapo itabaini kuna dalili ya watu kufanya mipango ya kuanzisha vurugu kwa kisingizoa cha dini.

"Serikali tumechua maamuzi mapya kuhusu suala kama hili, hapo mwanzo tulikuwa tunawakamata wale wanaoshiriki lakini sasa tutawakamata wale wote waliofanikisha, waliotekeleza na waliowatuma," alisema waziri Dk. Nchimbi.

Alisema uamuzi huo wa Serikali umechukuliwa kwa nia njema ya kutetea nchi isitumbukizwe katika vita vya kidini na watu wachache ambao aliwaita ni wahuni.

Alisema chanzo cha vurugu zilizofanyika Zanzibar na Dar es salaam hazina msingi wowote kwa sababu madai yaliyotolewa na watu wa Kikundi cha Uamsho kwa Zanzibar na Jumuiya za Taasisi za Kiislamu  kwa Tanzania bara hazina msingi na Serikali hausiki.

KIONGOZI WA UAMSHO ASHIKILIWA NA POLISI

Waziri Dk. Nchimbi alisema Jeshi la Polisi linamshikilia Kiongozi wa Kikundi cha Uamsho Sheikh Farid Hadi  kwa mahojiano ili ataje mahali alipokwenda baada ya kutoweka siku kadhaa na kusababisha wafuasi wake kufanya vurugu katika mitaa mbalimbali ya mji wa Zanzibar.

Alisema Serikali haikuhusika na kutoweka kwa kiongozi huyo ndio maana imeamua kumshikilia ili aeleze wapi alikuwa siku hizo, nia na madhumuni ya kutoweka huko.

"Kama mtu alitoweka ghafla na baadae anaonekana akinywa kahawa lazima Serikali ishtuke, tumeona lazima tumshikilie kwa mahojiano ili atuambie alikuwa wapi, nia ya kutoweka na madhumuni yake ili  umma uelewe," alisema Dk. Nchimbi.

Alisema Tanzania inaendeshwa kwa mujibu wa sheria na hakuna mtu ambaye hawezi kuguswa kwa kuhofia watu kufanya vurugu.

"Hatutabembelezana tena jambo kama hili, tufuate sheria na hakuna mtu ambaye atakuwa haguswi, tutamgusa na wale watakaoleta vurugu tutapambana naye," alisisitiza.

SHEIKH PONDA KAMWE HAACHIWI KWA MAANDAMANO.

Akizungumzia kuhusu suala la Sheikh Issa Ponda, Dk Nchimbi alisema wanaoleta vurugu kwa kushinikiza Sheikh Ponda kuachwa huru wamegonga ukuta kwa sababu tayari yupo katika mikono ya mahakama na hakuna mtu atakayeweza kumtoa nje.

Alisema kwenye vurugu zilizotokea jijini Dar es Salaam, baadhi wa wafuasi wake walikuwa wakiishinikiza Serikali kumtoa nje kiongozi huyo jambo ambalo kamwe halitawezekana.

Alisema kimsingi mahakama ndio yenye mamlaka ya kufanya hivyo kutokana na mipaka ya kiutendaji iliyopo kikatiba.

"Madai yao hayana msingi kwa sababu Sheikh Ponda amefikishwa mahakamani na hakuna mtu anayeweza kuingilia mahakama, wasubiri siku iliyopangwa kusikilizwa na kwa kesi hiyo pengine anaweza kuomba na kupewa dhamana," alisema.

NCHI IPO HATARINI

Hata hivyo Waziri Nchimbi alisema Watanzania wasikubali kuona watu wanataka kuweka nchi katika mpasuko wa kidini na kusababisha kuwepo kwa mauaji ya halaiki.

Alisema Serikali haitakubali kuona nchi inapoteza amani na utulivu uliojengwa kwa nguvu kubwa na waasisi wake Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Aman Karume kwa sababu vizazi vinavyokuja vitakuja kuwahukumu.

Alisema jukumu la Serikali iliyowekwa madarakani na wananchi kidemokrasia ni kuhakikisha nchi inakuwa tulivu na yenye amani, hivyo aliwataka wananchi wote kuunga mkono hatua zote za Serikali zitakazochukua katika kufanya wananchi wote wanaishi kwa udugu na ushirikiano kama zamani.

Dk Nchimbi alisema Serikali ipo tayari kukaa pamoja na vikundi mbalimbali vya kidini, taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali kujadili jambo hilo, lakini haipo tayari kufanya mazungumzo kwa shinikizo la mtu.




CHANZO: NIPASHE JUMAPILI

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundekadama@yahoo.com au WhatsaApp: + 255 757 478 553 au 0625 918 527

0/Post a Comment/Comments