Na Mwandishi wetu , Dodoma
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Mheshimiwa Dkt. Rhimo Nyansaho (Mb), amekutana na kufanya mazungumzo na Meja Jenerali Mstaafu Zawadi Madawili, mwanamke wa kwanza Afrika Mashariki kufikia cheo cha Meja Jenerali, katika ziara aliyomtembelea nyumbani kwake Upanga, jijini Dar es Salaam.
Ziara hiyo imefanyika Novemba 16, 2026, ikiwa na lengo la kumjulia hali Meja Jenerali Mstaafu Madawili pamoja na kubadilishana naye uzoefu kuhusu safari yake ya utumishi wa kijeshi na mchango wake katika kulinda na kuitumikia nchi.
Meja Jenerali Mstaafu Zawadi Madawili ana historia ya kipekee katika sekta ya ulinzi na usalama, kutokana na kuwa mwanamke wa kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki kufikia cheo cha Meja Jenerali, mafanikio yanayoakisi mchango wake katika utumishi wa kijeshi na kuvunja vikwazo vya wanawake katika nyanja ya uongozi wa kijeshi.
Katika mazungumzo hayo, Waziri Nyansaho alipata fursa ya kusikiliza uzoefu wa Meja Jenerali Mstaafu Madawili, mafanikio aliyoyapata katika kipindi cha utumishi wake pamoja na mambo muhimu yanayoweza kuwa funzo kwa kizazi cha sasa na kijacho katika utumishi wa kijeshi.
Aidha, ziara hiyo ni sehemu ya kutambua na kuthamini mchango wa viongozi waliolitumikia Taifa kwa uadilifu na kujitolea, huku historia ya Meja Jenerali Mstaafu Madawili ikiendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa wanawake wanaotamani kushiriki katika sekta ya ulinzi, usalama na uongozi wa kijeshi.


TAFUTA HABARI
Social Plugin