Habari Mpya

6/recent/ticker-posts

WAZIRI MCHENGERWA AWAALIKA WADAU KUSHIRIKI ASILI INVESTMENT GALA 2027



Waziri wa Afya, Mohamed Omary Mchengerwa, amewaalika wawekezaji, wadau wa tiba asili na sekta ya afya kushiriki katika dhifa ya uwekezaji wa tiba asili ijulikanayo kama Asili Investment Gala 2027, inayotarajiwa kufanyika Aprili 2027, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali za kuendeleza tiba asili na kuhakikisha inatambulika na kuunganishwa katika mfumo rasmi wa huduma za afya nchini.

Dhifa hiyo yenye kauli mbiu “Wekeza katika Dawa Zetu za Ndani za Tiba Asili” inalenga kuhamasisha uwekezaji na ushirikiano wa wadau katika uzalishaji wa dawa za tiba asili, tafiti, ubunifu na ujenzi wa uwezo wa rasilimali watu, ili kuendeleza sekta hiyo na kuongeza mchango wake katika huduma za afya.

Akizungumza na waandishi wa habari Novemba 19, 2026 Jijini Dar es Salaam, Mhe. Mchengerwa amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuhakikisha tiba asili inajumuishwa katika mfumo rasmi wa huduma za afya kufikia mwaka 2030, ikiwemo huduma za afya ya msingi na mipango ya Bima ya Afya kwa Wote, kwa kuzingatia sera, miongozo na taratibu zinazotumika nchini.

Amewataka wawekezaji na wadau mbalimbali kutumia fursa ya Asili Investment Gala kujitokeza, kushirikiana na kuwekeza katika sekta hiyo, huku akiwahimiza waganga na wadau wa tiba asili ambao hawajasajiliwa kukamilisha usajili wao mapema ili waweze kutambuliwa na kushiriki katika fursa za maendeleo ya sekta hiyo.

Aidha, amesema usajili na uthibitishaji wa dawa za tiba asili ni muhimu katika kuhakikisha ubora, usalama na ufanisi wa bidhaa, kwa kushirikiana na taasisi zinazohusika na udhibiti na usimamizi wa huduma za afya, ikiwemo TMDA, MSD na taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara ya Afya.

Kupitia dhifa hiyo, Wizara inalenga kujenga mazingira wezeshi ya uwekezaji na ushirikiano yatakayochochea maendeleo ya tiba asili, kuimarisha tafiti na ubunifu, pamoja na kuhakikisha tiba asili inapata nafasi katika mfumo rasmi wa huduma za afya nchini.

Download/Pakua/Install App ya Malunde 1 blog Google Playstore Bofya Hapa

Je, unayo taarifa ya kusisimua ambayo ungependa tuichapishe? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia malundeblog@gmail.com