Mamlaka ya Uwekezaji Tanzania - TISEZA imewataka wadau wanaotaka kuwekeza, wa ndani na nje ya nchi, kufika ofisini kwao ili kupewa maarifa ya kuwekeza katika mnyororo wa thamani katika sekta ya kilimo.Wito huo umetolewa na Meneja Uhamasishaji wa Uwekezaji wa Ndani ya Nchi wa TISEZA, Bwana Daudi Riganda, wakati akizungumza katika Maonesho ya Kimataifa ya HortiLogistica Africa 2026 yanayofanyika Jijini Arusha.
Amesisitiza kuwa fursa ya kuongeza thamani katika sekta ya kilimo ni kubwa, na bado haijatumika kikamilifu.
Amesema wawekezaji wameanza kuchangamkia fursa za miundombinu ya umwagiliaji, maghala na coldroom, lakini amesema fursa ya kuongeza thamani bado haijachangamkiwa ipasavyo.
Aidha, amesema kigezo kuhusu mtaji ni kiasi cha Shilingi za Kitanzania milioni 150 kwa mwekezaji wa ndani, wakati mwekezaji wa nje ni mara kumi ya mtaji wa mwekezaji wa ndani.
Ili kurahisisha uwekezaji, amesema kuna Kituo cha Huduma za Pamoja ambacho kinahusisha taasisi zaidi ya kumi na tano. Miongoni mwa taasisi hizo ni COPRA, TanTrade, ATO, TPHPA, TRA na TITEZA.
TITEZA ni miongoni mwa taasisi zilizohudhuria katika Maonesho hayo ya Kimataifa ya HortiLogistica, yanayofanyika kwa mara ya kwanza barani Afrika na kuhusisha nchi takribani 42 kutoka mabara ya Afrika, Asia na Ulaya.
Zaidi ya washiriki 3,000 wanatarajiwa kushiriki katika maonesho hayo yaliyoanza tarehe 8 Novemba na yanatarajiwa kuhitimishwa tarehe 10 Novemba 2026.
Aidha, nchi ya Tanzania imekuwa mwenyeji wa maonesho hayo ambayo kwa mara ya kwanza yamefanyika barani Afrika.

TAFUTA HABARI
Social Plugin